1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa OPEC nchini Angola

21 Desemba 2009

Shirika la nchi zinazouza mafuta duniani -OPEC- linakutana siku ya Jumanne nchini Angola, likitazamia kuendelea kutoa mafuta kwa viwango vilivyopunguzwa kwa dharura wakati wa msukosuko wa kiuchumi mwaka mmoja uliopita.

https://p.dw.com/p/LA8V

Kwa mara ya kwanza kabisa, mwenyeji wa mkutano huo wa OPEC ni Angola ambayo ni nchi mpya yenye utajiri mkubwa wa mafuta barani Afrika. Kwa maoni ya mawaziri wengi wa nchi wanachama wa OPEC, bei ya mafuta ya hivi sasa ya kama dola 75 kwa pipa ni bei muwafaka kwa wanachama wote 12. Hata hivyo wachambuzi wanasema, mawaziri wa mafuta wanaokutana hiyo kesho mjini Luanda watakuwa wakiikodolea macho sekta ya mafuta nchini Iraq inayoanza kuimarika pamoja na mipango yake ya kutazamia kuongeza viwango vya mafuta yanayochimbwa nchini humo kwa viwango vitakvyoweza hata kushindana na vile vya Saudi Arabia iliyo mtoaji mkubwa kabisa wa mafuta katika OPEC. Lakini waziri wa mafuta wa Iraq Hussein al-Shahristani alipozungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili alisema, yeye hatazamii kuzungumzia viwango vya Iraq. Akasisitiza kuwa Iraq inajikuta katika hali ya kipekee kwa sababu ni nchi inayoanza kuchipuka baada ya vita vya miaka. Kwa hivi sasa Iraq hailazimishwi kufuata viwango vilivyowekwa kwa azma ya kudhibiti bei ya mafuta duniani.

Waziri wa Mafuta wa Angola Jose Botelho de Vasconcelos amesema viwango vilivyokubaliwa vitabakia pale pale.Katika mwezi wa Januari,wanachama wa OPEC waliamua kupunguza kutoa mafuta kwa mapipa milioni 4.2 kila siku - hatua iliyosaidia kupandisha maradufu bei ya mafuta iliyoporomoka hadi kufikia dola 32 kwa pipa katika mwezi wa Desemba.

Hata hivyo mada inayotazamiwa kuwa na utata katika mkutano huo wa OPEC mjini Luanda ni utekelezaji wa viwango hivyo vilivyowekwa, kwani baadhi ya wanachama hivi karibuni, wametoa mafuta zaidi katika masoko ya dunia. Kinachohitajiwa ni kuheshimiwa zaidi viwango vilivyokubliwa amesema Waziri wa Mafuta wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mohammed bin Dhaen al-Hamli. Nchi inayopindukia sana viwango vilivyowekwa na OPEC ni mwanachama Angola ambayo ni mwenyeji wa mkutano wa hiyo kesho mjini Luanda na iliyoshika wadhifa wa urais unaozunguka katika OPEC. Iran na Nigeria ni wanachama wengine wanaopindukia viwango vilivyokubaliwa. Mtoaji mkubwa kabisa wa mafuta, Saudi Arabia ni nchi iliyopunguza sana pia viwango vya mafuta yanayochimbwa nchini humo katika jitahada ya kudhibiti bei ya mafuta katika masoko ya dunia.

Mwandishi: P.Martin/AFP/RTR

Mhariri: M. Abdul-Rahman