1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Repuplikan waelekezwa kwenye mkondo wake

19 Julai 2016

Mgombea urais wa Marekani Donald Trump amejaribu kuurudisha kwenye mkondo wake mkutano mkuu wa chama cha Repulican unaofayika Cleveland Marekani kwa ajili ya kumteuwa rasmi kama mgombea wa urais wa chama hicho.

https://p.dw.com/p/1JSCG
Picha: Reuters/M. Segar

Nje ya ukumbi wa mkutano katika mji wa Cleveland hapo Jumatatu usiku wafuasi wa Trump na wale wanaompinga walikabiliana huku vikosi vya usalama vikiwa vimesimama baina yao kuepusha uwezekano wa mapambano. Mgombea wa chama hicho anateuliwa katika mkutano huo mkuu na imetangazwa kwamba Trump atateuliwa kutokana na kupata ushindi wa wajumbe wengi katika majimbo kadhaa nchini Marekani.

Hadi mwishoni mwa juma kundi lenye kumpinga Trump ndani ya chama hicho limekuwa mbioni kujaribu kulazimisha marudio ya kura ya jimbo kwa jimbo jambo ambalo lingelipelekea kumnyima Trump uteuzi wa moja kwa moja kutoka mkutano huo mkuu wa chama.

Katika dalili ya kuendelea kuwepo mgawanyiko ndani ya chama hicho vigogo waandamizi wa chama hicho ukiwemo ukoo mzima wa akina Bush,aliyeteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho hapo mwaka 2008 Mitt Romney na hata gavana alioko madarakani wa jimbo la Ohio lenye kuandaa mkutano huo John Kasich ambaye alikuwa ziarani Cleveland wameususia mkutano huo.

Tutashinda kwa vishindo

Trump mwenyewe binafsi alijitokeza katika mkutano huo wa uteuzi hapo jana na kuvunjilia mbali desturi za jadi za uteuzi kwa kuwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba watashinda kwa vishindo

Donald Trump katika mkutano mkuu wa chama chake cha Repuplikan.
Donald Trump katika mkutano mkuu wa chama chake cha Repuplikan.Picha: Reuters/R. Wilking

Mkutano huo hakuanza vyema hapo jana baada ya wajumbe wanaompinga Trump kunyimwa fursa ya kuzungumza na wakawa wanahanikiza kwa sauti za kuzomea.

Tunastahiki kusikilizwa huu ni mkutano wa wananchi ametamka hayo Diana Shores mjumbe kutoka Virginia wakati wajumbe wanaomuunga mkono Trump wakipiga mayowe ya "aibu,aibu!"

Wengi walikasirika kwamba chama cha akina Abraham Lincoln na Teheodore Roosevelt (marais mashuhuri wa zamani wa Marekani) kitaongozwa na mtu ambaye anawaita Wamexico kuwa ni wabakaji pamoja na kupendekeza kuwazuwiya Waislamu kuingia nchini Marekani.

Matakwa ya wanachama yaheshimiwe

Wafuasi wa Trump wamekuwa wakisisitiza kwamba wajumbe waheshimu matakwa ya wanachama wa chama hicho kuwa kumfanya Trump kuwa mgombea wao ambapo suala la uhamiaji lilitamalaki wakati wa ufunguzi wa mkutano huo mkuu wa chama hapo jana.

Donald Trump na mke wake Melania Trump katika mkutano mkuu wa chama chake cha Repuplikan.
Donald Trump na mke wake Melania Trump katika mkutano mkuu wa chama chake cha Repuplikan.Picha: picture-alliance/abaca

Mmojawapo aliyechangia alikuwa ni Sabine Durfen mwanasheria mwenye kupigania mageuzi ya uhamiaji ambaye mwanawe wa kiume aliuwawa katika ajali ya gari lililokuwa likiendeshwa na mhamiaji aliyekuwa akiishi Marekani kinyume na sheria.

Durfen amekaririwa akisema "Hillary Clinton au kama vile tunjuavyo "Bazazi Clinton" siku zote amekuwa akizungumzia kile atakachokifanya kwa wageni walioko nchini kinyume na sheria na kile atakachofanya kwa wakimbizi.Donald Trump anazungumzia juu ya kile atakachofanya kwa Marekani."

Tajiri huyo mkubwa wa Marekani Donald Trump alikuwa amejipatia ushindi mkubwa katika uchaguzi wa chama wa majimbo kadhaa kwa kukujisanyia kura zaidi ya milioni 13 ambazo hazikuwahi kufikiwa kabla na mgombea yoyote yule wa chama cha Repuplikan.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri :Josephat Charo