1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Ulaya na Mediterania

B.Riegert / P.Martin7 Novemba 2007

Mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi za Umoja wa Ulaya na nchi za eneo la Bahari ya Mediterania wamemaliza mkutano wao wa siku mbili katika mji mkuu wa Ureno Lisbon wakiwa na matarajio mema.Mada kuu iliyojadiliwa ni mchakato wa amani katika Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/C7f5

Ushirikiano kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na za eneo la Mediterania unajulikana pia kama Utaratibu wa Barcelona baada ya kuzinduliwa mwaka 1995 katika mji wa Barcelona nchini Uhispania.Azma ni kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Safari hii pia,mawaziri wa nje wa Umoja wa Ulaya walipokutana na mawaziri wenzao kutoka nchi za mashariki na kusini mwa Mediterania pamoja na pia viongozi wa Kipalestina,mada iliyopata kipaumbele ni mzozo wa Mashariki ya Kati.Na kwa mujibu wa Javier Solana-mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya,hilo wala halishangazi.Akaongezea hivi:

„Kumbuka kuwa hakuna ko kote kwengine ambako Waisraeli na Wapalestina hukutana pamoja na Waarabu na Wazungu kama hapa.“

Wakati huo huo Waziri wa Nje wa Israel Tzipi Livni aliitumia fursa ya mkutano huo kuzungumza na wajumbe wa Kipalestina na hata mawaziri wa nje wa nchi za Kiarabu,kwani Israel haina uhusiano wa kibalozi na nchi hizo.Na kuhusu mkutano wa amani wa Mashariki ya Kati unaotazamiwa kufanywa Annapolis nchini Marekani Livni amesema:

„Israel haitoweka masharti ya kushiriki mkutano wa Annapolis,kwa sababu utaratibu huo ni sehemu ya maslahi yetu.Tunaamini kuwa tunapaswa kuwapa matumaini Waisraeli na Wapalestina vile vile.“

Akaongezea kuwa Israel ipo tayari kufanya majadiliano ya dhati na inataraji kuwa Wapalestina pia watakwenda mkutanoni bila ya kuweka masharti hapo kabla.

Kwa upande mwingine Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu,Amr Moussa hana hakika ikiwa mkutano wa Annapolis utaweza kuanza.Akaendelea kusema:

„Kwanza hebu tuwape Wapalestina na Waisraeli nafasi ya kama siku 10 au majuma 2 kuendelea na majadiliano na kupata waraka utakaowawezesha kwenda mkutanoni.“

Hata hivyo majadiliano ya mjini Lisbon yalikuwa na utata kwa sababu viongozi wa Kipalestina hawana mamlaka katika Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na kundi la Hamas lenye itikadi kali za Kiislamu.Hamas huishambulia Israel kwa makombora kutoka eneo hilo.Israel na wajumbe wa Kipalestina wanalenga kuwa na mataifa mawili huru yenye usalama wa mipakani.