1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa umoja wa Afrika wajaribu kuepuka mgawanyiko kuhusu Zimbabwe.

Kitojo, Sekione1 Julai 2008
https://p.dw.com/p/EULR
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe katika mkutano wa viongozi wa Afrika mjini Sharm El Sheikh nchini Misr.Picha: AP



Mkutano  wa  umoja  wa  Afrika  mjini  Sharm El Sheikh  nchini  Misr  leo  umekuwa  ukijaribu kujiepusha  na  mgawanyiko  juu  ya  vipi  viongozi wa  nchi  hizo  wanaweza  kulishughulikia  suala  la kuchaguliwa  tena  rais  Robert  Mugabe  katika uchaguzi  ambao  umeshutumiwa  duniani  kote.


Sekione  Kitojo  anaichunguza  hali  hiyo.



Duru   katika   mkutano  huo  zinasema   kuwa viongozi  wamegawanyika  baina  ya  wale  ambao wanataka  kutoa  matamshi  makali  juu  ya Zimbabwe  na  wengine  ambao  wanasita  sita  kutoa matamshi  hayo  hadharani  na  kumshutumu kiongozi  huyo  mkongwe, ambaye  amerefusha utawala  wake  wa  miaka  28  katika  uchaguzi ambapo  alikuwa  mgombea  pekee  Ijumaa  iliyopita.

Rais  wa  Sierra  Leone , Ernest  Bai  Koroma , ambaye  ni  mmoja  kati  ya  kundi  la  viongozi  wa mataifa  ya  Afrika  magharibi   na    mashariki  ambao ni  wakosoaji  wakubwa  wa  rais  Mugabe, amesema kuwa   watu  wa  Zimbabwe  wamenyimwa  haki  yao ya  kidemokrasia. Tunapaswa, bila  kujali  chochote kushutumu  kile  kilichotokea.

Koroma  amesema  kuwa  kundi  la  mataifa  ya kusini  mwa  Afrika  ni  lazima  wawashirikishe Mugabe  na  Tsvangirai , ambaye  alijitoa  katika uchaguzi  kutokana  na  kushambuliwa  na  vitisho dhidi  ya  wafuasi  wa  chama  chake, katika mazungumzo yatakayoleta  serikali  ya  mpito pamoja  na  uchaguzi  mpya.

Lakini  msemaji  wa  rais  Mugabe  George Charamba   amekataa  wazo  la  kuwa  na  suluhisho kama  la  Kenya  la  kuwa  na  mpango  wa kugawana  madaraka  serikalini, mpango  ambao umedokezwa  na   viongozi  kadha  katika  mkutano wa  viongozi  wa  Afrika,  ili  kumaliza  mzozo  ambao umeikabili  Zimbabwe  pamoja  na  hali  mbaya  ya kiuchumi   pamoja   na  mataifa  ya  jirani  kutaabika kuwahifadhi  mamilioni  ya   wakimbizi  katika  nchi zao.Katika  shutuma  zake  Charamba  amemlenga zaidi  waziri  mkuu  wa  Kenya  Raila  Odinga.

Chama  cha  Movement for  Democratic  Change kimepinga  ripoti  moja  ya  gazeti  la  Afrika  kusini kuwa  mpatanishi  mkuu  wa  mzozo  wa  Zimbabwe rais  Thabo  Mbeki  wa  Afrika  kusini  alikuwa  yuko karibu  na  kupata  makubaliano  kutoka  kambi  ya Mugabe  na  Tsvangirai   kuweza   kujadili  kuhusu serikali  ya  umoja  wa  kitaifa.

Katibu  mkuu  wa  chama  cha  MDC Tendai  Biti , ambaye  ametoka   kifungo  kwa  dhamana kuhusiana  na   kesi  ya  uhaini  dhidi  yake, amesema   kuwa  ukweli  ni  kwamba   hakuna mazungumzo  yoyote  ama  majadiliano yanayofanyika  baina  ya  pande  hizi  mbili  na muhimu  zaidi , hakuna  makubaliano  yoyote yanayotarajiwa.

Biti  amesema   kuwa  wakati  chama  cha  MDC kilikuwa  kinatafuta   njia  ya  majadiliano   katika juhudi  za   kuunda  serikali  ya   umoja  wa  kitaifa kabla  ya  Juni 4, uchaguzi   wa  bandia  uliofanyika wa  duru  ya  pili Juni  27,  umeondoa  kabisa uwezekano  wowote  wa  kupata  suluhisho  kwa  njia ya  majadiliano.

►◄