1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya ushirikiano wa Kusini na Kusini wamalizika leo.

Kabogo Grace Patricia2 Desemba 2009

Mkutano huo unaofanyika mjini Nairobi, Kenya unawashirikisha viongozi wa juu wa umoja huo katika mataifa ya Kusini na Kusini

https://p.dw.com/p/Kp9R
Makamu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha Rose Migiro.Picha: AP

Mkutano wa viongozi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ushirikiano wa Kusini na Kusini mwa dunia, umeanza mjini Nairobi, Kenya, huku Makamu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha Rose Migiro akitoa wito wa kupatikana kwa ufumbuzi unaofaa na kuimarisha ushirikiano huo wa Kusini na Kusini na ule wa Kaskazini na Kusini mwa dunia ili kukabiliana na mahitaji ya dunia ambayo yanategemeana. Mkutano huo wa siku tatu unaomalizika hii leo, unazungumzia na kutilia mkazo ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi ndani ya dunia inayoendelea kama vile nchi za Kusini mwa dunia kuwa na nafasi za uongozi katika kushughulikia masuala ya duniani ikiwemo usalama wa chakula, mabadiliko ya hali ya hewa na maradhi ya kuambukizi. mkutano huo pia utapitia tena maendeleo ya miaka 30 tangu mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya ushirikiano wa kiufundi miongoni mwa mataifa yanayoendelea uliofanyika mjini Buenos Aires, Argentina mwaka 1978. Edward Sambili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango na Maendeleo ya Taifa nchini Kenya, anasema matatizo katika nchi zinazoendelea ni rahisi kutatulika kuliko matatizo katika mataifa yaliyoendelea. Kwa upande wake mkurugenzi wa idara maalum ya ushirikiano wa Kusini na Kusini katika Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, Yiping Zhou anasema ushirikiano wa biashara ya Kusini na Kusini ni muhimu. Biashara ya Kusini na Kusini imeongezeka kwa kiwango cha asilimia 13.4 kwa mwaka toka mwaka 1995 na kufikia dola trilioni 2.4 ambayo ni sawa na asilimia 20 ya biashara ya dunia kwa mwaka 2007. Asilimia 40 ya biashara duniani kwa sasa inatokana na masoko yanayoibukia na mataifa yanayoendelea.

Ujumbe wa Ban Ki-moon

Akiwasilisha salamu za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, Bibi Asha Rose Migiro alisema maendeleo hayapatikani katika eneo ambako hakuna mikakati ya kuongeza biashara ya kuvuka mipaka na uwekezaji. Kwa mujibu wa Bwana Ban, nchi zinazoendelea pia zimekuwa zikiongezeka umuhimu wake kutokana na kuwa vyanzo kwa mataifa yaliyoendelea. Anasema endapo ahadi zinazotolewa zitafanikishwa mtiririko jumla wa biashara huenda ukafikia dola bilioni 15 kwa mwaka ujao. Mzozo wa kiuchumi unaoendelea kwa sasa umeongeza idadi ya watu wanaoishi chini ya kiwango cha umasikini katika mataifa yanayoendelea na nyingi ya nchi hizo haziko katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia ifikapo mwaka 2015. Akisisitizia juu ya hilo, bibi Ann Dismorr Balozi wa Sweden nchini Kenya na muakilishi wa Umoja wa Ulaya wakati nchi yake ikiwa mwenyekiti wa sasa wa umoja huo, amesema mzozo wa kiuchumi unaoikabili dunia unayawekea malengo ya maendeleo ya milenia katika hatari na jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuzidi kuziunga mkono nchi zinazoendelea na jitihada katika kuyafikia malengo hayo. UNDP ina lengo la kuunga mkono jitihada na mikakati inayofanywa na mataifa ya Kusini na Kusini katika kupata maendeleo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (IPS)

Mhariri:Abdul-Rahman