1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa UNCTAD mjini Accra

Miraji Othman22 Aprili 2008

Licha ya kwamba sisi wanadamu wote tunaishi katika sayari ile ile moja inayoitwa DUNIA, hata hivyo, hatuko katika hali ya usawa pale kila mmoja wetu anapolipia bei ya vyakula.

https://p.dw.com/p/Dm8w
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-MoonPicha: DW

Hivi sasa katika mji mkuu wa Ghana, Accra, unafanyika mkutano wa Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya Biashara na Maendeleo, UNCTAD, ambao unatakiwa utafute njia ya kuweko mfumo wa usawa katika kukigawa chakula kilioko duniani. Mkutano huu unafanyika huku kukiweko hofu duniani kote ya ukosefu na ughali wa bei za vyakula pamoja na mishtuko mikubwa katika taasisi za kifedha za kimataifa. Utandawazi, nafasi zilioko na mitihani ilioko mbele yetu ndio kauli mbiu ya mkutano huu wa UNCTAD utakaoendelea wiki hii yote, na ambao unafanyika miaka minne tangu ule wa Brazil. Nchi zinazoendelea zina matumaini makubwa juu ya kile ambacho kitafikiwa, hasa kuhusu mzozo wa sasa wa uhaba wa vyakula duniani, kam vile nafaka, kusambaratika masoko ya fedha pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Yote hayo ni mambo yaliofungamana, hasa ilivokuwa dunia yetu sasa imekuwa kama kijiji.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, katika ufunguzi wa mkutano huo, alisema :

+Kwa mujibu wa Shirika la Mipango ya Vyakula Duniani, bei za mazao muhimu ya vyakula kutoka kilimo na nafaka nyingine zimepanda zaidi ya nusu mnamo miezi sita iliopita. Sababu za mzozo huu ni nyingi na haziwezi tu, kama wengine wanavosema, kutajwa kwamba zinatokana na kubadilishwa mazao ya kilimo kuwa nishati. Bei kubwa ya mafuta imezidisha garama za kilimo; na kuyasafirisha mazao hayo ya kilimo pamoja na uzalishaji wa vyakula umeathirika mwaka huu kutokana na ukame na maafa mengine ya kimaumbile. Kupanda uchumi kumezidisha ulaji wa mazao ya kilimo, hasa barani Asia; ulanguzi katika mifumo ya kubadilisha sarafu na kuanguka muda mrefu bei ya sarafu ya dola ya Kimarekani, huenda kuwa ndio sababu. Jambo moja ni hakika katika miaka mitatu iliopita, nalo ni kwamba dunia imetumia vyakula vingi zaidi kuliko vile ilivolima.+

Katibu Mkuu huyo aliuwambia mkutano wa karibuni wa bodi ya Shirika la UNCTAD kwamba jamii ya kimataifa ina jukumu maalum la kuipeleka hali ilioahidiwa karibuni ya kupanda uchumi hadi katika nchi zilizo na umaskini wa kupindukia. Alisema mkutano wa Accra lazima uandae mkakati barabara wa kuupiga jeki utandawazi, kuendeleza biashara na uwekezaji ili umaskini upunguzwe na uchumi upande. Bwana Ba Ki-Moon alisema mchango wa Umoja wa Mataifa ni kuutumia utandawazi ili kuupunguza umaskini, akiashiria kwamba mwaka 2008 utawashughulikia watu bilioni moja walio katika tabaka ya umaskini wa kupindukia, kwa vile utandawazi umewaacha nyuma watu hao, hasa katika nchi za Afrika chini ya Jangwa la Sahara.

Malengo ya ya Millennium yaa Umoja wa Mataifa ya kuupunguza umaskini kwa nusu ifikapo mwaka 2015 hayatafikiwa kwa viwango vya sasa vya maendeleo.

Waziri wa Ghana wa biashara na sekta ya kibinafsi, Joe Baidoe-Ansah, alisema mkutano huu wa Ghana utawawezesha wenye kutoa maamuzi kuyashughulikia masuala muhimu ya sasa kama vile nishati, uhamiaji na kuchomoza nchi zinazoendelea kama injini za kukuza uchumi. Bila ya shaka, nchi wanachama wa UNCTAD zinatakiwa ziyatambuwe majibu ya kisiasa yanayofaa pamoja na hatua gani zinazofaa kuchukuliwa.

Bila ya shaka, mkutano wa UNCTAD nchini Ghana unatoa nafasi kwa bara la Afrika kumurikwa na kujulikana michango yake katika uchumi wa dunia na pia kuyazusha masuala yalio muhimu kwa nchi za Kiafrika, hasa ukitilia maanani kwamba kuna malalamiko mingi kwamba watu wa Afrika hawapati sehemu yeyote ya faida zinazotokana na utandawazi.

Jarida la la ECONOMIST la Uengereza limeielezea hali ya sasa ya kupanda juu sana bei za vyakula duniani kuwa ni Tsunami ya kimya kimya. Hasa katika nchi zinazoendelea, watu wako kwenye shida kubwa kutokana na bei kubwa ya vyakula na nishati. Hali hiyo imesababishwa hasa na mahitaji makubwa ya nafaka huko Uchina na India, kwa vile nchi nyingi maskini zinazidi kutegemea vyakula vya kutoka nchi za nje.

Katibu Mkuu wa UNCTAD, Sipatchai Panitchpakdi, alisema:

+Nafikiri sasa hatua ya haraka lazima ichukuliwe. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Vyakula Duniani na Benki ya Dunia zinachukua hatua ya pamoja ya kutoa fedha za kutosha. Mzozo wa chakula unaweza ukafanya umaskini katika nchi nyingi kuwa mbaya zaidi.+

Inajulikana kwamba ruzuku zinazotolewa na serekali za nchi za viwanda kwa wakulima wao ndio moja wapo ya sababu ya hali hii ya sasa. Mazao ya bei rahisi kutoka Ulaya na Marekani yanafanya kilimo katika nchi nyingi zinazoendelea kwenda chini. Na zaidi katika miaka iliopita, misaada ya maendeleo katika sekta za kilimo imepungua, hali ambayo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema lazima ibadilike ili kwamba katika siku za mbele nchi ziweze zenyewe kujikimu kwa vyakula:

+Lazima kuweko uwiano ulio bora zaidi katika juhudi zetu za kutoa misaada, kufanya biashara na kusamehe madeni. Tangu nilipokamata madaraka ya ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nimejitahidi sana kuona kwamba Umoja wa Mataifa unafanya kazi kwa ufanisi zaidi ambapo siasa ya maendeleo inapewa kipa umbele. Lazima tupimwe kutokana na matokeo ya vitendo vyetu, na sio kutokana na maneno yetu.+

Uwazi ni kwamba ni muhimu Shirika la UNCTAD liwe na uwezo zaidi katika hali ya sasa ya nchi kuzidi kutegemeana. Ikumbukwe kwamba katika miaka mitano tu iliopita, nchi zinazoendelea zimejionea uchumi wao ukipanda kwa asilimia tano au zaidi kila mwaka, na dunia imeshuhudia kuchomoza nchi zenye uzito wa kiuchumi, nje ya nchi za viwanda za Magharibi, kama vile Uchina, India na Brazil.

Na bila ya shaka, matokeo yanatakiwa yaonekane kwa haraka, kwani hali ilivyo sasa ni ya kutia wasiwasi. Kumetokea michafuko katika nchi nyingi duniani, Misri, Burkina faso, Ivory Coast, Philippines, Haiti tusiisahau, kutokana na kupanda juu bei za vyakula. Na inakubalika kwamba kupanda juu sana kwa bei za vyakula kunahatarisha utulivu katika nchi kadhaa katika Afrika na kwengineko. Huu mkutano wa Accra utatwama katika kujiuliza: kwanini nchi tajiri ndizo zinazofaidika na utandawazi, lakini sio nyingi ya nchi zilizo maskini? Na kwanini katika nchi ile ile ambayo inatajwa kwamba uchumi wake umepanda kwa kiasi, lakini umaskini ndani ya nchi hiyo haujapungua?

Hata hivyo, lazima sisi wanadamu tusiweke matumainio yetu makubwa juu ya mkutano huu wa UNCTAD wa Accra, kama alivosema Detlef Kotte, mkuu wa idara ya uchumi na mbinu za siasa za maendeleo wa Shirika la UNCTAD:

+Lazima mtu aseme wazi kwamba Accra sio jukwaa la kutia saini mikataba na maamuzi ya mwisho kufikiwa. Lakini mkutano huu una umuhimu mkubwa hasa katika wakati huu, licha ya kwamba ni mkutano wa kawaida unaotakiwa kufanyika kila miaka minne. Unaangukia katika wakati ambao ni muhimu katika kuonyesha mkondo utakaoendea maamuzi, mashauriano ya biashara, kuiondoa mizozo ya sasa kwa wakati mfupiu jao, athari za muda wa wastani kwa mfumo wa kiuchumi wa kimataifa na vipi yatafanyika marekebisho ndani ya taasisi za kifedha za kimataifa.+

Yakipatikana hayo, hiyo itakuwa hatua kubwa mbele.