1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Usalama wafunguliwa Munich

N.Werkhäuser - (P.Martin)6 Februari 2009

Mkutano wa usalama unaofunguliwa leo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier mjini Munich,ni mkutano unaoheshimiwa mno kuhusu sera za usalama.

https://p.dw.com/p/GoHu
Steinmeier
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier.

Kuanzia leo hadi Jumapili ijayo mamia ya wataalamu wa masuala ya ulinzi na usalama na wanasiasa wa ngazi ya juu watakusanyika Munich kusini mwa Ujerumani. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ni miongoni mwa viongozi hao.Hotuba itakayotolewa na Makamu mpya wa Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Jumamosi inangojewa kwa hamu.

Mkutano wa Usalama wa Munich kila mwaka hufanikiwa kuvutia viongozi mashuhuri.Na mwaka huu mgeni mashuhuri kabisa ni Makamu mpya wa Rais wa Marekani Joe Biden atakaeeleza sera za serikali mpya ya Marekani kuhusu ushirikiano wake na Ulaya na pia dhima itakayotimizwa na nchi hiyo katika NATO.Bila shaka macho yote yatamkodolea Biden atakapoeleza hali ya Afghanistan ambako Marekani inataka kuimarisha idadi ya majeshi yake.Nchi za Ulaya mkutanoni,hasa zitataka kujua iwapo Washington inatazamia mchango zaidi kutoka washirika wake wa Ulaya. Miongoni mwa viongozi watakaoisikiliza hotuba ya Biden kwa makini ni Rais wa Afghanistan Hamid Karzai,anaegombea tena uchaguzi katika mwezi wa Agosti.Inavyoonekana,hakuna hakika kuwa safari hii Marekani itamuunga mkono Karzai kugombea tena uchaguzi huo. Ni dhahiri kuwa wajumbe wa Afghanistan na Marekani watakuwa na masuala kadhaa ya kujadiliwa pembezoni mwa mkutano wa usalama mjini Munich.

Lakini haielekei kuwa kutafanywa mkutano wa ana kwa ana kati ya Biden na wajumbe wa Iran yaani Waziri wa Mambo ya Nje Manouchehr Mottaki na Rais wa Bunge Ali Larijani.Kimsingi,pendekezo la kufanywa majadiliano lililotolewa na serikali mpya ya Marekani huiingiza Iran pia.Ni matumaini ya Elke Hoff mwanasiasa wa Kijerumani anaehusika na masuala ya usalama kuwa majadiliano ya mradi wa nyuklia wa Iran yatafufuliwa hivi karibuni.Hoff amesema,mkono ulionyoshwa na serikali ya Obama kuarifu kuwa ipo tayari kwa majadiliano ya uso kwa uso,ni njia pekee iliyo ya maana.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Steinmeier katika hotuba yake ya ufunguzi atazungumzia suala la kuzuia usambazaji wa silaha za kinyuklia na hapo bila shaka Iran itatajwa.Kwa maoni yake utaratibu wa kinyuklia unapswa kuwa chini ya usimamizi wa kimataifa.Hilo si jingine isipokuwa kuhakikisha kuna usimamizi wa kimataifa kokote kunapotumiwa teknolojia ya kurutubisha madini. Kwa maoni yake ,usimamizi huo uwe chini ya shirika la kimataifa la IAEA. Steinmeier atakutana na Mkuu wa shirika hilo Mohammed El Baradei mwishoni mwa juma hili mjini Munich.