1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa mataifa kuhusu malengo ya maendeleo ya millenia

Oumilkher Hamidou20 Septemba 2010

Katibu mmkuu wa Umoja wa mataifa anawasihi viongozi wa dunia wazidishe juhudi zao kuhakikisha malengo ya maendeleo ya millenia yanafikiwa ifikapo mwaka 2015

https://p.dw.com/p/PHgX
Viongozi wanaohudhuria mkutano wa Umoja wa mataifa kuhusu malengo ya maendeleo ya Millenia mjini New YorkPicha: AP

Viongozi wa taifa na serikali za nchi wanachama wa Umoja wa mataifa wanakutana hii leo kutathmini malengo ya maendeleo ya Millenia ya kupunguza kwa nusu hali ya umaskini ulimwenguni hadi ifikapo mwaka 2015.

Mbali na kupunguza hali ya umaskini uliokithiri,malengo mengine ya maendeleo ya Millenia yaliyowekwa mwaka 2000 ni pamoja na kuhakikisha elimu msingi kwa wote,kuendeleza haki sawa za kijinsia,kupunguza idadi ya vifo vya watoto,kuimarisha afya ya wakinamama,kupiga vita ukimwi,malaria na maradhi mengineyo,kuhifadhi mazingira na kubuni ushirika kwaajili ya maendeleo ulimwenguni.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon akifungua mkutano huo hii leo ameutolea mwito ulimwengu uwajibike zaidi ili kuyafikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa.

Amekadiria zaidi ya dola bilioni mia moja zitahitajika kuweza kugharimia malengo ya maendeleo ya millenia.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amesema:

"Inasikitisha zaidi kuona kwamba kule ambako mahitaji ni makubwa zaidi ndiko kwenye uhaba mkubwa zaidi."

Millenniums-Gipfel
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-MoonPicha: AP

Katika hati iliyoandaliwa na ambayo inatazamiwa kuidhinishwa hadi jumatano ijayo,viongozi wa taifa na serikali wanaelezea masikitiko yao kuona jinsi idadi ya watu wanaoishi katika hali ya ufukara au wanaosumbuliwa na njaa ilivyoongezeka na kupindukia watu bilioni moja na tatizo linalotokana na ukosefu wa usawa kati ya nchi na nchi ,sawa na katika maeneo ya ndani ya nchi linavyozidi kukua.

"Mgogoro wa kiuchumi umezidisha idadi ya wenye kuweza kudhurika,umezidisha pengo kati ya wanaojimudu na wasiojimudu na umevuruga maendeleo yaliyoweza kupatikana"-hati hiyo inasema.

Licha ya hali ngumu ya kiuchumi,viongozi katika mkutano huo wa siku tatu wa kilele wanatazamiwa kuelezea matumaini yao kuona malengo ya maendeleo ya millenia yanafikiwa ifikapo mwaka 2015.

Matumaini kama hayo yameelezewa pia na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon katika hotuba yake ya ufunguzi hii leo mjini New-York.

Hata hivyo baadhi ya wataalam wanashuku kama malengo yote hayo manane yataweza kufikiwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Viongozi 140 wa taifa na serikali,akiwemo kansela Angela Merkel, wanatazamiwa kuhutubia mkutano huo.Rais Barack Obama wa Marekani anatazamiwa kuhutubia jumatano,siku ya mwisho ya mkutano huo .

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman