1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa wafadhili mjini Islamabad

Oumilkher Hamidou21 Mei 2009

Pakistan yaahidiwa zaidi ya dala milioni 220 kuwahudumia wakimbizi

https://p.dw.com/p/HukU
Watoto wa kipakistan katika kambi za wakimbizi za Umoja wa mataifaPicha: picture alliance / landov

Waziri mkuu wa Pakistan Yusuf Raza Gilani ameitolea mwito jumuia ya kimataifa iisaidie kukabiliana na kishindo kikubwa kabisa kinachotokana na mikururo ya watu zaidi ya milioni mbili walioyapa kisogo maskani yao kutokana na mapigano ya jeshi la serikali dhidi ya wataliban.

Hujuma za jeshi zilizoanza karibu mwezi mmoja uliopita katika bonde la Swat na vitongoji vyake katika eneo la kaskazini magharibi zimewatimua karibu raia milioni moja na nusu ,wengi kati yao wamejazana katika kambi za mahema.

Wamekuja kuchanganyika na wengine laki tano waliokimbia mapigano kati ya wanaharakati wa kiislam wanaoshirikiana na Al Qaida na wanajeshi katika maeneo ya kikabila ya kaskazini magharibi-karibu na mpaka wa Afghanistan.

Serikali ya mjini Islamabad imeonya ikiwa wakimbizi hao hawatoshughulikiwa,kuna hatari ya kutangamia kutokana na kusonga mbele wafuasi wa itikadi kali.

"Ni muhimu kwa wale wanaotaka kupambana na ugaidi,kutoa jibu la pamoja na la jumla kwa suala hili"-amesema waziri mkuu Yusuf Raza Gilani,alipokua akifungua mkutano wa wafadhili katika mji mkuu wa Pakistan-Islamabad.

Kwa kuwasaidia wakimbizi,tunawazuwia wafuasi wa itikadi kali wasiitumie hali yao na kujipendekeza-tunalazimika kupata imani ya wakimbizi"-amesisitiza waziri mkuu huyo.

Washirika wa Pakistan kutoka zaidi ya nchi 40 wanaonyesha kuitika mwito huo . Wameahidi hii leo kutoa msaada wa zaidi ya dala 220 milioni kuwahudumia wakimbizi hao.

Waziri wa fedha wa Pakistan,Hina Rabbani Khar ameuambia mkutano na waandishi habari wafadahili wameahidi dala milioni 224,ikiwa ni pamoja na dala milioni 110 zilizoahidiwa jumanne iliyopita na Marekani.

Zaidi ya fedha hizo, Marekani imetuma ndege mbili za kijeshi zilizosheheni mahema yenye mitambo ya hewa ya baridi na vyakula vilivyokwisha pikiwa karibu na mji mkuu Islamabad.Shehena nyengine ya misaada kama hiyo inatazamiwa kupelekwa leo.

"Tunaridhika sana na jibu hilo-amesema waziri huyo wa fedha,bibi Hina Rabbani Khar.

Umoja wa mataifa unapanga kutoa mwito kesho wa kukusanya jumla ya dala milioni 600 kuwahudumia wakimbizi.

Pakistan yenyewe imetenga msaada wa dharura wa rupia milioni mbili kwa sasa-kiwango ambacho ni sawa na dala milioni 25-na ambacho wachunguzi wa kimataifa wanahisi ni haba kupita kiasi.

Wengi miongoni mwa waliokimbia mapigano, vyombo vya habari vya Pakistan na mashirika ya kimataifa ya haki za binaadam,wanalilaumu jeshi kwa kuripua mabomu mtindo mmoja tangu hujuma hizo zilipoanza April 26 iliyopita na kuwauwa raia kadhaa wasiokua na hatia.Duru hizo hizo zinawalaumuu pia wataliban kwa kuwatumia raia kama ngao dhidi ya mashambulio ya jeshi la serikali.

Shirika la Umoja wa mataifa la Mpango wa chakula ulimwenguni,limeonya jana,fedha zilizopo zitatosha kuwahudumia wakimbizi hadi kati kati ya mwezi July tuu.

Mwandishi :Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul Rahman