1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa benki ya Afrika ajibu madai dhidi yake

Saumu Mwasimba
28 Mei 2020

Rais wa benki ya maendeleo ya Afrika AfDB Akinwumi Adesina amejibu madai yanayomuandama ya rushwa na ameapa kuendelea kufanya kazi.

https://p.dw.com/p/3cueK
Akinwumi Adesina, neuer Präsident der Afrikanischen Entwicklungsbank
Picha: AFP/Getty Images/S. Kambou

Siku ya Jumatano katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Adesina alijibu vikali kuhusu kile alichokiita majaribio ya kutungwa na baadhi ya watu kumchafulia sifa yake na kusema ataendelea kufanya kazi na kila mtu na kila mwenye hisa.

Marekani inatia msukumo wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu madai yaliyotolewa na wafichua siri ambayo yametajwa na jopo la uchunguzi la ndani kwamba hayakubainika.

Imedaiwa kwamba chini ya rais huyo wa benki ya maendeleo ya Afrika Adesina umefanyika ubadhirifu wa fedha pamoja na upendeleo. Adesina anawania muhula wa pili wa miaka mitano wa nafasi hiyo ya taasisi muhimu barani Afrika.

Adensina amesema hana hatia kuhusiana na madai yaliyotolewa ambayo yanawania kinyume cha sheria kumuondolea hadhi yake na uadilifu pamoja na kuichafua sifa ya benki hiyo ya Afrika.

Kofi Annan
Amemtaja Koffi Annan kama mmoja wa mashujaa wake.Picha: DW/P. Musvanhiri

Amewataja Nelson Mandela rais wa zamani wa Afrika Kusini na Kofi Annan aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kama mashujaa wake ambao maisha yao yameonesha kwamba mtu anaimarika kwa kupitia uchungu.

Akasema ana imani kwamba mchakato wa usawa,uwazi na wa haki utafanyika kwa kuheshimu sheria,miongozi na mifumo ya usimamizi ya benki hiyo na utawala wa sheria kuthibitisha kwamba hajakiuka kanuni yoyote ya maadili ya taasisi hiyo.

Adesina ni mnigeria wa kwanza kushikilia uongozi wa benki ya AfDB mojawapo ya taasisi tano kubwa za maenedeleo duniani.

Alikuwa waziri wa kilimo wa Nigeria akijulikana sana kwa unadhifu wake lakini pia kwa utaratibu wake wa usimamizi ambao wakosoaji waliuangalia kama ni wa kiimla.

Ikumbukwe kwamba benki hiyo ya maendeleo ya Afrika ilitikiswa na msururu wa kuondoka kwa maafisa kadhaa wa ngazi za juu punde alipoingia Adesina mwenye umri wa miaka 60 katika uongozi wa chombo hicho.

Uchaguzi wa rais mpya wa benki hiyo uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi huu wa Mei sasa utafanyika mwezi Agsti na Adesina ni mgombea pekee katika kinya'ng'anyiro hicho. Anaungwa mkono na Umoja wa Afrika,na Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Ukanda wa Afrika Magharibi ECOWAS.