1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa utawala wa Khmer Rouge, Cambodia ahukumiwa

Josephat Nyiro Charo26 Julai 2010

Mahakama ya uhalifu wa kivita inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa leo imemhukumu mkuu wa zamani wa jela ya mateso wakati wa utawala wa Khmer Rouge nchini Cambodia, Kaing Guek Eav kifungo cha miaka 30 jela

https://p.dw.com/p/OUkX
Kaing Guek Eav, mkuu wa utawala wa zamani wa Khmer Rouge, CambodiaPicha: AP

Kaing Guek Eav amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kivita na utesaji mwishoni mwa miaka ya 1970. Eav ni afisa wa kwanza wa kijeshi wakati wa utawala huo kuhukumiwa na mahakama hiyo ya kimataifa.

Kaing Guek Eav anayejulikana zaidi kama Duch amehukumiwa kifungo hicho cha miaka 30 jela kwa kuhusika na mauaji ya watu hadi milioni mbili kwa kuwanyonga, kuwashindisha na njaa na kuwatumikisha kupita kiasi. Awali Eav, mwenye umri wa miaka 67 alihukumiwa kifungo cha miaka 35 jela, lakini mahakama hiyo ikapunguza adhabu hiyo kutokana na mtuhumiwa huyo kushikiliwa kwa miaka kadhaa katika jela ya kijeshi kinyume cha sheria kabla mahakama hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa haijaanzishwa.

Wakati kesi hiyo inasikilizwa katika mahakama hiyo ya Phnom Penh, Eav alikiri kuhusika na uhalifu huo na aliomba msahama kwa kuhusika na mauaji ya kiasi watu 15,000, wanauame, wanawake na watoto katika jela ya Tuol Sleng ambayo pia inajulikana kama S-21. Lakini mwezi Novemba, Eav aliishangaza mahakama hiyo baada ya kuomba aachiliwe huru.

Eav, mwalimu wa zamani wa somo la hisabati amehukumiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu na uhalifu wa kivita. Jaji mkuu wa mahakama hiyo, Nil Nonn alisema hukumu hiyo imetolewa kutokana na ushahidi ulitolewa na mshtakiwa mwenyewe, watu waliosalimika na mauaji wakati wa utawala huo na pamoja na vyama vya kiraia.

Umati wa watu wa Cambodia, wekiwemo watu walionusurika kuuawa wakati wa utawala huo, walikusanyika katika mahakama hiyo iliyojengwa kwenye viunga vya mji wa Phnom Penh wakiwa na matumaini ya kuona haki ikitendeka dhidi ya makosa yaliyofanywa na utawala wa Khmer Rouge kuanzia mwaka 1975 hadi 1979.

Waendesha mashitaka waliiomba mahakama hiyo isiyo na uwezo wa kutoa adhabu ya kifo, imhukumu Eav kifungo cha miaka 40 jela. Eav aliyekuwa amevalia fulana ya rangi ya buluu aliingizwa katika mahakama hiyo na gari lililokuwa na vioo vya rangi nyeusi vya kuzuia risasi kwa lengo la kuwadhibiti watu walionusurika kuuawa wakati wa utawala huo wasilipize kisasi. Eav anashitakiwa pamoja na viongozi wengine wanne ambao kwa pamoja watafunguliwa mashitaka ya mauaji ya halaiki mwanzoni mwa mwaka ujao.

Utawala huo ulioongozwa na Pol Pot, ulihusika na kuwaua karibu robo ya idadi ya watu wa nchi hiyo na kuyafanya mauaji hayo yawe ya kutisha katika karne ya 20. Utawala wa Khmer Rouge uliondolewa madarakani na vikosi vya jeshi vilivyoungwa mkono na Vietnam mwaka 1979, lakini vita vya wenyewe kwa wenyewe viliendelea hadi mwaka 1998. Pol Pot alikufa mwaka huo huo.

Eav amekuwa akishikiliwa tangu mwaka 1999, wakati alipokutwa akifanya kazi kama mfanyakazi wa shirika la misaada la Kikristo katika msitu na alikamatwa rasmi na mahakama hiyo Julai mwaka 2007. Mahakama hiyo pia inachunguza iwapo ifungue kesi zaidi dhidi ya maafisa wengine watano wa jeshi wakati wa utawala wa Khmer Rouge baada ya kuzuka ubishi kati ya waendesha mashitaka wa kimataifa na wale wa Cambodia kuhusu iwapo wawafungulie mashitaka watuhumiwa wengine.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Mtullya.