1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mlindalango wa Schalke 04 Manuel Neuer kuhamia Bayern Munich

2 Juni 2011

Bayern imesema Neuer atajiunga na timu hiyo Julai mosi na atafanyiwa uchunguzi wa kiafya baada ya michuano ya timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani kutafuta nafasi ya kufuzu kwa mashindano ya kombe la Ulaya 2012

https://p.dw.com/p/11Syu
Kipa wa Schalke 04, Manuel NeuerPicha: picture alliance/dpa

Kipa wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani, Manuel Neuer, ambaye pia ni mlinda lango wa timu ya Schalke 04, atajiunga na timu ya Bayern Munich mwezi ujao kwa mkataba wa miaka 5, mara tu uchunguzi wa kitabibu utakapokamilika. Mkataba wa kumhamisha Neuer kutoka Schalke 04 hadi Bayern ulisainiwa jana (01.06.2011) Taarifa ya Bayern imesema Neuer atajiunga na timu hiyo Julai mosi na atafanyiwa uchunguzi wa kiafya baada ya michuano ya timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani kutafuta nafasi ya kufuzu kwa mashindano ya kombe la Ulaya 2012 - "Euro 2012".

Manuel Neuer, mwenye umri wa miaka 25, ambaye alijiunga na Schalke 04 tangu alipokuwa na umri wa miaka 5, aliisaidia timu hiyo kushinda kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani msimu huu na pia kufika nusu fainali ya kinyang'anyiro cha ubingwa wa Ulaya. "Nina matarajio makubwa kwa changamoto hii na ya kusisimua ya kuichezea Bayern," amesema Neuer baada ya kumaliza shakashaka zilizokuwepo kuhusiana na mustakabali wake katika soka. "Nitacheza katika timu moja pamoja na wachezaji wenzangu wa timu ya taifa, kwa hiyo hayatakuwa mazingira mageni kwangu," ameongeza kusema .

Hata hivyo Manuel Neuer anatakiwa kutarajia baadhi ya washabiki wa Bayern kugadhabishwa na uamuzi wake kwa kuwa walijaribu mara kwa mara kuzuia kuhamishwa kwa mchezaji mwingine, Ralf Faerhrmann, wanayemuona kuwa nyota wa wapinzani wao katika Bundesliga, Schalke 04. Faerhrmann, mwenye umri wa miaka 22, aliihama Eintracht Frankfurt baada ya timu hiyo kushuka daraja kutoka ligi ya Bundesliga, na kuchukua nafasi ya Manuel Neuer kama mlindalango wa Schalke 04.

Neuer anatazamwa kuwa miongoni mwa walindalango mahiri barani Ulaya na kulikuwa na tetesi kwamba angejiunga na timu ya Manchester United ya England.

Wakati huo huo uongozi wa Bayern Munich umetangaza kumsajili mlinzi wa timu ya taifa ya kandanda ya Brazil, Rafinha kutoka kwa klabu ya Genoa ya Italia, kwa mkataba wa miaka 3. Bayern sasa inajiwinda kulitwaa kombe la mabingwa wa Ulaya kwa kuwa sasa imempata Manuel Neuer na Rafinha.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri:Abdul-Rahman