1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mlolongo wa mikutano juu ya mzozo wa kifedha

Nijimbere, Gregoire19 Oktoba 2008

Viongozi wa Marekani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya, wamependekeza mlolongo wa mikutano duniani juu ya mzozo wa kifedha wa hivi sasa.

https://p.dw.com/p/Fcql
Rais wa Marekani George W.Bush na rais wa Ufaransa Nicolas SarkozyPicha: AP

Rais wa Marekani, George W. Bush, rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, na rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso, wamesema baada ya mkutano wao huko Camp David Marekani kuwa watawasilisha fikria ya kuandaa mlolongo wa mikutano ya kuusuluhisha mgogoro wa kifedha wa hivi sasa kwa viongozi wengine wa dunia wiki ijayo. Mikutano hiyo itaanza baada ya uchaguzi wa rais wa Marekani uliyopangwa kufanyika tarehe 4 mwezi ujao.

Katika taarifa ya pamoja, viongozi hao wamesema mkutano wa kwanza utafanyika nchini Marekani na utakadiria hatua imekwishafikiwa katika kupambana na mgogoro wa kifedha wa hivi sasa na utatafuta kufikia makubaliano juu ya mageuzi yanayohitajika ili kuepusha mgogoro kama huo kutokea tena na kuhakikisha ukuaji wa uchumi mnamo miaka ijayo. Rais Bush anaamini hatua zinazochukuliwa zitazaa matunda. Rais Bush alisema:

'' Tunashughulikia tatizo kubwa. Lakini raia wa Marekani na raia wengine duniani, wajuwe kuwa tuna imani kuwa hatua tunazozichukuwa zitafanya kazi''.

Hata hivyo, rais George W. Bush anaonya juu ya kile amekitaja athari ya kuvuruga msingi wa mfumo wa uchumi wenye soko huru, na uwekezaji ambao anasema ulifanikisha kukua uchumi duniani licha ya matatizo ya kifedha ya hivi sasa. Amesema mazungumzo katika mikutano hiyo ijayo itafanyika katika kuhakikisha kuwa msingi huo wa kiuchumi umehifadhiwa vyema ila ziwekwe sheria za kuulinda mfumo wa kifedha duniani ambao ni dhamana kwa uchumi.