1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mmoja auawa na 25 wajeruhiwa Cairo

Thelma Mwadzaya23 Februari 2009

Nchini Misri washukiwa watatu wamekamatwa na polisi nchini humo kufuatia shambulio la bomu lililotokea kwenye soko moja mjini Cairo

https://p.dw.com/p/GzUr
Mtaa wa soko la Khan al Khalili mjini CairoPicha: dpa


Mlipuko huo umesababisha kifo cha mtu mmoja raia wa Ufaransa na 25 wamejeruhiwa wengi wao watalii.Shambulio hilo la jana Jumapili ni la kwanza kutokea dhidi ya raia wa kigeni tangu mwaka 2006.Hata hivyo hakuna kundi lolote lililokiri kuhusika katika shambulio hilo.


Shambulio hilo lilitokea kwenye soko la Khan al -Khalili lililokuwa na mikahawa mingi.Soko hilo la kihistoria ni kivutio kikubwa cha watalii na limekuwako kwa kipindi cha miaka 1,500.

Kulingana na afisa mmoja wa polisi watu watatu wanaoshukiwa kuhusika na shambulio hilo tayari wamekamatwa na mashahidi wengine bado wanaendelea kuhojiwa.


Msichana wa kiFaransa aliye na umri wa miaka 17 alifariki hospitalini kwasababu ya majeraha aliyoyapata.Dada huyo alikuwa katika kundi la watalii 54 waliotokea eneo la Paris walioshukia mtaa huo kwa lengo la kununua zawadi za tunu kabla ya kurejea nchini mwao.Kulingana na maafisa wa serikali wa Misri na Ufaransa watalii wenzake 17 walijeruhiwa katika shambulio hilo.Mmoja wa waliokuwa safarini alieleza kuwa ulisikika mlipuko mkubwa uliofuatiwa na mayowe na vurumai.

Kwa mujibu wa naibu waziri wa Afya wa Misri Nasir Rasmi aliyezungumza na shirika la habari la AFP watalii wengine watatu waliojeruhiwa ni pamoja na raia mmoja wa Kijerumani aliye na umri wa miaka 37,Wasaudia watatu na waMisri wanne.

Damu ilitapakaa katika eneo la msikiti wa zamani wa Hussein baada ya purukushani hiyo.Kulingana na walioshuhudia tukio hilo shambulio hilo lilisababisha majengo yaliyokuwa karibu kutikisika.

Wahudumu wa afya walionekana kuwa katika pilika pilika za kuwafikisha majeruhi hospitalini.Watalii hao walikuwa wamepanga kurejea nchini Ufaransa hii leo baada ya kukamilisha ziara yao ya Cairo.

Kwa upande mwengine bado haijabainika jinsi shambulio hilo lililivyotokea.Kwa mujibu wa waliolishuhudia na afisa mmoja wa polisi mabomu mawili yalirushwa kutokea paa moja la nyumba iliyokuwa karibu na barabara hiyo.Hata hivyo duru za polisi zinaeleza kuwa bomu moja pekee ndilo lililolipuka.

Taarifa nyengine zinaeleza kuwa mwanadiplomasia mmoja wa kigeni aliyeandamana na majeruhi hadi hospitalini aliwaeleza wachunguzi wa polisi kuwa walirushiwa mabomu hayo yaliyotokea kwenye paa la nyumba moja iliyokuwa karibu.

Mbunge mmoja wa Misri aliye pia mwanachama wa kamati ya bunge ya usalama wa kitaifa alikanusha taarifa hizo na kueleza kuwa bomu hilo la kutengezwa nyumbani liliwekwa chini ya ubao wa saruji wa kukakalia ndipo likalipuka.

Mabomu hayo yalilipuka nje ya hoteli ya Al-Hussein iliyo karibu na msikiti wa Hussein.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar kilichoko mjini Cairo Sheikh Mohammed Sayyed al-Tantawi aliyepia kiongozi wa kidini wa KiSunni wa ngazi za juu alilaani vikali shambulio hilo.

Shambulio hilo lililowalenga watalii ni la kwanza kutokea tangu mwaka 2005 ambapo watalii 18 walijeruhiwa katika mtaa huohuo mjini Cairo.

Msururu wa milipuko ya mabomu ilitokea kwenye rasi ya Sinai kati ya mwaka 2004-2006 na kusababisha vifo vingi vya watalii waliokuwa kwenye hoteli zilizo karibu na bahari ya Sham.Wapiganaji wanaoliunga mkono kundi la Al Qaeda wanaripotiwa kuhusika na shambulio hilo.

Itakumbukwa kuwa katika miaka ya 1990 Misri ilikabiliwa na mashambulio ya mabomu yaliyowalenga watalii wa kigeni jambo lililoathiri sekta ya utalii inayotegemewa nchini humo.Sekta hiyo iliyo na asilimia 12.6 ya wafanyakazi wote ilipata dola bilioni 11 kwasababu ya watalii milioni 13 waloiizuru Misri mwaka jana pekee.

AFPE