1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mnangagwa ashinikiza Mugabe ajiuzulu

Grace Kabogo
21 Novemba 2017

Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyefukuzwa kazi, Emmerson Mnangagwa, amemtaka Rais Robert Mugabe kuachia madaraka akisema atarejea nchini humo iwapo atahakikishiwa usalama wake.

https://p.dw.com/p/2nycR
Kombobild Mnangagwa (l) Mugabe (r)
Picha: AP

Mnangagwa ambaye ametoa wito huo leo, anaungana na viongozi wa kijeshi pamoja na wanasiasa, wanaomtaka Rais Mugabe aheshimu maoni ya umma na kuondoka madarakani, ili nchi hiyo iweze kusonga mbele na kulinda hadhi yake. Mnangagwa ambaye kwa sasa hayuko Zimbabwe, amesema aliondoka nchini humo kwa sababu maisha yake yalikuwa hatarini baada ya kufukuzwa katika chama tawala cha ZANU-PF.

Amethibitisha kuwa Mugabe amemualika arejee nyumbani kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusu hali ya kisiasa ilivyo Zimbabwe, lakini amekataa wito huo hadi hapo atakapohakikishiwa usalama wake. Katika taarifa yake, Mnangagwa ambaye inaaminika atakuchukua nafasi ya Mugabe, ameongeza kusema kuwa kutokana na matukio yaliyotokea baada ya kufukuzwa kwake, hawezi kumuamini tena Mugabe.

Jana usiku jeshi la Zimbabwe lilisema Mnangagwa atarejea nchini humo hivi karibuni na amekuwa akiwasiliana na Mugabe. Katika taarifa hiyo, Mkuu wa Majeshi Jenerali Constantino Chiwenga aliwaambia waandishi habari kwamba hatua imepigwa kuelekea kufikia makubaliano na amewasihi wananchi kuwa watulivu.

Simbabwe Veteranen fordern Rücktritt von Mugabe
Maveterani wa vita wa ZimbabwePicha: Getty Images/AFP/J. Nijkizana

Hatua ya kufukuzwa Mnangagwa ilisababisha jeshi la Zimbabwe kuchukua udhibiti wa madaraka wiki iliyopita. Mnangagwa anaungwa mkono na jeshi pamoja na maveterani wa vita wenye ushawishi mkubwa, wote hao ambao walikuwa na hofu huenda Mugabe mwenye umri wa miaka 93, anaweza akakabidhi madaraka kwa mkewe, Grace Mugabe.

Hayo yanajiri wakati ambapo maveterani wa vita wameitisha maandamano ya dharura kwa lengo la kumpinga Rais Mugabe. Mwenyekiti wa umoja wa maveterani, Chris Mutsvangwa amewataka wananchi kuandamana hadi kwenye makaazi binafsi ya Mugabe, yanayojulikana kama Blue Roof, ili kuhakikisha kwamba kiongozi huyo anayeendelea kutengwa, anaondoka haraka madarakani.

Mugabe kuondolewa kisheria

Wakati huo huo, wabunge wa ZANU-PF wanajiandaa kuanzisha mchakato wa kumuondoa kisheria madarakani Rais Mugabe, baada ya kupuuza muda wa mwisho uliowekwa ajiuzulu. Afisa habari wa chama hicho, Simon Khaya Moyo amewaambia waandishi habari kwamba Mugabe tayari amearifiwa kuhusu hatua hiyo leo asubuhi.

'' Kutokana na hilo, chama kimemuamuru kiongozi wa wabunge kuendelea na mchakato wa kisheria kumuondoa madarakani komredi Robert Mugabe kwa sababu hatujapokea uthibitisho wowote kutoka kwa spika wa bunge, kuhusu kujiuzulu kwake,'' amesema Moyo.

Simbabwe Parlament in Harare Vereidigung
Wabunge wa ZimbabwePicha: AP

Aidha, wabunge hao wamewataka mawaziri wa serikali kususia mkutano wa baraza la mawaziri ulioitishwa leo na Mugabe Ikulu. Siku ya Jumapili, Mugabe hakujiuzulu wakati alipolihutubia taifa kwa njia ya televisheni. Muda wa mwisho ambao chama hicho kilikuwa kimempa Mugabe awe amejiuzulu, ulimalizika jana mchana.

Ama kwa upande mwingine, nchi nne za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, zinakutana leo ili kuuzungumzia mzozo wa kisiasa wa Zimbabwe. Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma anahudhuria mkutano huo ulioandaliwa na Angola, pamoja na viongozi wa Zambia na Tanzania. Kamati ya SADC, imependekeza mkutano wa kilele wa mataifa yote wanachama 16 kujadiliana kuhusu Zimbabwe.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf