1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moamer Kadhafi achaguliwa mwenyekiti mpya wa umoja wa Afrika

Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP2 Februari 2009

Kiongozi wa libya Moamer Kadhafi amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika katika mkutano wa kilele wa mataifa 53 wanachama mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

https://p.dw.com/p/Glsv
Rais wa Libya Moamer KadhafiPicha: AP


Punde baada ya kuchukua wadhifa huo aliapa kuhimiza kuundwa serikali moja ya bara la Afrika swala ambalo halijaungwa mkono na viongozi wengi wa bara hilo.

Kadhafi alichaguliwa mwenyekiti katika mkutano wa faragha, kufuatia kura iliyopigwa na viongozi kutoka mataifa 53 wanachama. Katika hotuba yake ya ufunguzi kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 66 alisema anatumai wakati akishikilia nafasi hiyo kwa muda wa mwaka mmoja hatakuwa kiongozi wa maneno matupu bali vitendo.


Alisema ataendelea kuyashinikiza mataiafa ya bara la Afrika kubuni mikakati itakayofanikisha kuundwa kwa serikali moja ya bara hilo,japokuwa alikiri kuwa baadhi ya viongozi hawako tayari kuunga mkono wazo hilo.


Kadhafi ni miongoni mwa viongozi wa bara la afrika ambao wamekuwa madarakani kwa miaka mingi.Kiongozi huyo aliingia madarakani 1969 akiwa na umri wa miaka 29 kufuatia mapinduzi ya kijeshi.


Kabla ya mkutano huu wa Addis Ababa Kadhafi alikuwa ameyatembelea mataifa kadhaa kutafuta kuungwa mkono katika wadhifa wa mwenyekiti. Anachukua nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kutoka kwa rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.


Kiongozi huyo wa Libya kwa miaka mingi alikuwa ametengwa na mataifa ya magharibi kufuatia madai ya kuhusika katika visa vya kigaidi,ikiwemo kuhusika kwa taifa lake mwaka 1988 katika shambulizi la bomu katika ndege ya marekani katika naga ya Lockerbie na kusababisha vifo vya watu 270.


Kiongozi huyo wa Libya ndiye muasisi wa kubadilishwa kwa umoja wa zamani wa nchi huru za Afrika OAU 2001 na kuwa umoja wa Afrika mwaka 2001. Katika mkutano huo wa Addis Ababa kadhafi alishinikiza kuwepo kwa uhusiano wa karibu miongoni mwa mataifa wanachama kwa kuunda mamlaka mpya ya Umoja wa Afrika, itakayochukua nafasi ya tume ya Umoja huo.


Maswala mengine yaliyojitokeza katika mkutano huo wa mataifa 53 wanachama wa umoja wa Afrika ni ongezeko biashara haramu ya madawa ya kulevya hasa katika mataifa ya magharibi mwa Afrika. Kwa mujibu wa wataalam wa umoja wa mataifa wa kukabiliana na biashara haramu ya madawa ya kulevya makundi ya wafanyibiashara wenye ushawishi mkubwa kutoka Colombia walio na mitandao kote duniani wamekuwa wakiingiza katika mataifa hayo yakaribia tani 50 za coicane kila mwaka na mara mbili ya kiasi hicho yanaingia katika mataifa ya ulaya.


Katibu mkuu wa Umoja wa matifa Ban Ki-Moon ameuambia mkutano huo kuwa biashara hiyo imekuwa changamoto kuu kwa usalama na utawala katika mataifa ya magharibi.