Modric ndiye mchezaji bora wa mwaka duniani

Mchezaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia Luka Modric ameshinda tuzo ya mchezaji soka bora duniani Ballon d'Or, na kutilia kikomo miaka kumi ambayo tuzo hiyo ilitawaliwa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Modric mwenye umri wa miaka 33 alikuwa nguzo wakati Real Madrid waliposhinda taji lao la tatu mfululizo la Ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya msimu uliopita na alitajwa kuwa mchezaji bora kwenye Kombe la Dunia huko Urusi ambapo aliiongoza timu yake ya taifa kufika fainali kwa mara ya kwanza ambapo walibwagwa na Ufaransa.

Mchezaji wa mwisho kuishinda tuzo hiyo mbali na Messi na Ronaldo ambao wameshinda mara tano kila mmoja, alikuwa Ricardo Kaka wa Brazil mwaka 2007. Modric amemshinda Ronaldo ambaye ameichukua nafasi ya pili kisha wa tatu akawa mshambuliaji wa Atletico Madrid na Ufaransa Antoine Griezmann. Kylian Mbappe ambaye jana alishinda tuzo ya mchezaji bora chini ya miaka 21 alikuwa wa nne kisha Messi akaichukua nafasi ya tano.


Maudhui Zinazofanana

Tufuatilie