1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Gedi ataka jeshi la kulinda amani litumwe Somalia

14 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCSE

Wanaume wenye silaha mjini Mogadishu wanakodishwa kwa dola 2 za kimarekani kwa siku kama maofisa wa usalama wa kukabiliana na machafuko ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu takriban 25 katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Umoja wa Mataifa umeonya juu ya ongezeko la machafuko kwa kutokuwepo utawala mjini Mogadishu kulikosababishwa na kufurushwa kwa wanamgambo wa mahakama za kiislamu na majeshi ya Ethiopia. Katika ripoti yake iliyotolewa leo, Umoja la Mataifa pia umeonya juu ya kurejea tena kwa wababe wa kivita mjini Mogadishu.

Ongezeko la machafuko huenda likadumaza juhudi za kupeleka jeshi la kulinda amani Somalia litakalokuwa pia na kibarua cha kuilinda serikali iliyo dhaifu na kutoa mafunzo kwa jeshi jipya la nchi hiyo. Waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Somlia, Ali Mohamed Gedi, ametoa mwito jeshi la kulinda amani lipelekwe Somalia.

´Tunaitolea mwito jumuiya ya kimataifa na hususan Umoja wa Afrika utume wanajeshi wa kulinda amani nchini Somalia.´

Waziri Gedi amesema serikali yake imeliimarisha jeshi la polisi ili kuwalinda raia wanaokabiliwa na kitisho cha mahakama za kiislamu pamoja na washirika wake wa kigaidi.

Bwana Gedi amethibitisha kuna juhudi za maksudi zinazofanywa na wapiganaji katika maeneo kadhaa ya Somalia ili kuvuruga amani. Aidha amesema yanayoendelea mjini Mogadishu ni ishara dhahiri kwamba kuna baadhi ya watu ambao hawako tayari kuikubali amani kwa faida ya Wasomali.