1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Mapambano yapamba moto

26 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCg0

Ndege za kivita za Ethiopia zimeshambulia kwa mabomu viwanja viwili vya ndege mjini Mogadishu vinavyodhibitiwa na Uongozi wa Kiislam nchini humo wakati wapiganaji hasimu wakiendelea kupambana katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Ndege hizo za Ethiopia zimeushambulia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mogadishu pamoja na uwanja mwengine mkubwa kabisa wa kijeshi nchini Somalia ulioko kusini magharibi mwa mji mkuu wa Mogadishu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni jaribio la kuzuwiya kuletewa silaha kwa wapiganaji wa Kiislam ambao takriban wanadhibiti Somalia nzima.

Hata hivyo muda mfupi baada ya kushambuliwa kwa uwanja wa Mogadishu viongozi wa Kiislam Sheikh Hassan Dahir Aweys na Sheikh Sharif Ahmed walitua kwenye uwanja huo kutoka mahala kusikojulikana na hiyo kuashiria kwamba njia ya kurukia na kutua ndege ya uwanja huo haukuharibiwa sana.

Mapigano ya mizinga yameripotiwa karibu na mji wa Baidoa mji pekee ambao unadhibitiwa na serikali ya mpito ya Somalia. Serikali pia imetangaza kufungwa kwa mipaka yote ya ardhini ya Somalia,baharini na ile ya anga.Ethiopia na hasimu wake mkuu Eritrea ambayo inaelezwa kuunga mkono Uongozi wa Kiislam nchini Somalia zinakadiriwa kuwa na jumla ya hadi wanajeshi 20,000 nchini humo.

Hofu imekuwa ikizidi kuongezeka kwamba mzozo huo utakuja kusambaa eneo zima la Pembe ya Afrika.