1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Serikali ya mpito yatakiwa kuacha kutumia nguvu

25 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC7G

Ujerumani ikiwa ndio mwenyekiti wa sasa wa umoja wa ulaya imeitaka serikali ya Somalia kujizuia kutumia nguvu katika kampeni yake dhidi ya wapiganaji wa mahakama za kiislamu.

Balozi wa Ujerumani nchini Kenya bwana Walter Lindner amemuandikia barua rais wa Somalia Abdullahi Yusuf kuhusu kuacha matendo yasiyokubalika na wakati huo huo ameitaka serikali ya mpito ya Somalia kuruhusu misaada ya chakula na madawa iwafikie mamia ya watu wanayoihitaji.

Awali mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada yalitamka juu ya hali ya usalama inayozidi kuzorota nchini Somalia kwamba italeta maafa makubwa kwa binadamu.

Shirika la kimataifa la Madaktari wasio na mipaka limesema kwamba kuna hofu ya kuzuka mkurupuko wa ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa mengine ya kuambukiza katika kambi za wakimbizi wanaotoroka mapigano nchini Somalia.

Umoja wa mataifa umesema takriban watu laki tatu wameukimbia mji mkuu wa Mogadishu

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa umoja huo, mapigano yaliyotokea katika mji mkuu wa Mogadishu ni mabaya zaidi kuwahi kutokea katika muda wa miaka 16 iliyopita.