1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Mashambulio Mogadishu watatu wauawa

4 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBux

Majeshi ya shirika ya Ethiopia na Somalia yamewauwa raia watatu na kujeruhi wengine watano baada ya msafara wao kushambuliwa na guruneti mjini Mogadishu.Hilo ni shambulio la pili dhidi yao ambalo halikufanikiwa katika mkoa wa kaskazini wa Huriwa.Shambulio hilo linatokea siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Somalia Ali Mohamed Gedi kuponea chupuchupu pale gari lake lililoshambuliwa na mlipuaji wa kujitolea muhanga.

Bado haijajulikana aliyetekeleza shambulio hilo lililosababisha vifo vya walinzi wake sita.Yote hayo yanatokea baada ya mashambulio mwishoni mwa wiki katika eneo la kaskazini mashariki la Somalia baina ya majeshi ya usalama na wapiganaji wa kiislamu wanaodaiwa kuhusika na kundi la Al Qaeda.

Majeshi ya Ethiopia yakishirikiana na ya Somalia yaliwafurusha wapiganaji wa mahakama za kiislamu mwanzoni mwa mwaka na kupambana nao tena mwezi Machi na Aprili katika barabara za mji wa Mogadishu.Juhudi za kurejesha serikali nchini humo bado hazijafua dafu tangu Siad Barre kungolewa madarakani mwaka 91.