1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 15 wameuawa na wengine 70 kujeruhiwa, Nairobi

Shisia Wasilwa
28 Juni 2018

 Watu 15 wameuawa na wengine 70 kujeruhiwa, baada ya moto mkubwa kuteketeza soko la Gikomba na nyumba kadhaa jijini Nairobi nchini Kenya Alhamisi asubuhi. Moto huo ulianza majira ya saa 8:30 asubuhi na kusambaa.

https://p.dw.com/p/30SlR
Kenia Brand auf Markt Gikomba in Nairobi
Picha: Reuters/T. Mukoya

Watu 15 wameuawa na wengine 70 kujeruhiwa, baada ya moto mkubwa kuteketeza soko la Gikomba na nyumba kadhaa jijini Nairobi nchini Kenya Alhamisi asubuhi.

Mratibu wa jimbo la Nairobi Kengethe Thuku amesema kuwa moto huo ulianzia kwenye karakana ya mbao.

Moto huo ulianza majira ya saa 8:30 asubuhi na kusambaa katika soko hilo kubwa kabisa mjini Nairobi, na kuenea katika majengo yaliyokaribu na mitaa ya mabanda. Baadaye moto huo, ulidhibitiwa baada ya dakika 90 kwa mujibu wa Shirika la Huduma ya Dharura la St John Ambulance.

Gikomba ni soko kubwa Afrika Mashariki na Kati

Soko la Gikomba lililoko katikati mwa jiji la Nairobi kuliko na watu wengi, linategemewa na watu wengi wanaochuma riziki yao mahala hapo. Bidhaa za mitumba huuzwa pamoja na vipuri vya magari katika katika soko hilo ambalo linategemewa pia na raia kutoka mataifa ya Afrika Mashariki. Hii sio mara ya kwanza kwa soko hilo kuharibiwa na moto.

Soko la Gikomba
Soko la Gikomba Picha: picture-alliance/dpa/D. Irungu

Thuku anasema kuwa idadi ya watu walioaga dunia kutokana na moto huo uliotokea Alhamisi asubuhi imefikia 15.

"Watu karibu watano... walifikishwa hospitalini wakiwa maiti, lakini tungali na miili mingine tisa katika majengo yaliyoteketezwa kwa sababu tunataka kuthibitisha na kuhakikisha usalama wa majengo hayo," alisema.

Baadhi ya waathiriwa walipelekwa katika hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta (KNH) huku mwengine wa 15 aliyeaga dunia akipelekwa katika Hospitali ya Mama Lucy.

Watu wengine 70 walijeruhiwa kwenye mkasa huo wa moto ambao chanzo chake bado hakijabainishwa, alisema Thuku.

Mpiga picha wa shirika la Reuters aliona miili ikiondolewa kwenye jengo moja huku moshi mkubwa ukifuka mahala pa mkasa huo.

Kaimu mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa ya Kenyatta, Thomas Mutie alisema "iwapo tutapokea visa zaidi basi tumejiandaa vya kutosha."

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Reuters, Dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga