1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpambano wa kuwania madaraka Uingereza

Admin.WagnerD30 Juni 2016

Chama kikuu cha upinzani nchini Uingereza cha Labour kinaingia katika mpambano wa kuwania uongozi, kikiakisi mpambano uliopo katika chama tawala cha Kihafidhina, baada ya uamuzi wa kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya wiki.

https://p.dw.com/p/1JGer
Großbritannien Theresa May
Theresa May mgombea katika wadhifa wa mkuu wa chama cha ConservativePicha: Getty Images/C. Court

Angela Eagle , mbunge mwandamizi wa chama cha Labour , atatangaza leo Alhamis kwamba atapambana na kiongozi wa chama hicho Jeremy Corbyn ambaye amekuwa akikabiliwa na uasi unaoongezeka ndani ya chama chake cha Labour, ripoti za vyombo vya habari zimesema jana.

Eagle, waziri wa zamani anayehusika na masuala ya wastaafu , alijiondoa kuwa afisa wa juu wa chama cha Labour anayehusika na masuala a biashara siku ya Jumanne, mmoja kati ya watu 20 wa ngazi ya juu waliojiuzulu kutoka katika kikosi cha Corbyn cha sera za upinzani.

Großbritannien Michael Gove mit Ehefrau Sarah Vine
Michael Gove (kulia) mmoja kati ya wagombea wa chama cha ConservativePicha: Getty Images/J. Taylor

Miongoni mwa wahafidhina, mpambano wa kuwania madaraka tayari umeshaanza baada ya waziri mkuu David Cameron kuchukua hatua baada ya kipigo kibaya wiki iliyopita katika kura ya maoni kuhusu kubakia ama kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya na kutangaza kwamba anajiuzulu.

Waanza kutangaza nia

Waziri wa zamani wa ulinzi , Liam Fox , amesema atatangaza nia yake ya kuwania kiti hicho leo, wakati Boris Johnson , kiongozi wa kampeni iliyoshinda ya kujitoa, katika kura ya maoni , pia nae anatarajiwa kuthibitisha kujitupa ulingoni kuwania kiti hicho.

Hasimu mkubwa wa Johnson kuongoza chama cha Conservative na kuchukua wadhifa wa waziri mkuu anaonekana kuwa ni Theresa May, waziri wa mambo ya ndani , ambaye alikuwa katika kambi ya kubakia.

Großbritannien Liam Fox
Liam Fox amejitokeza nae kuwania wadhifa wa chama cha ConservativePicha: Getty Images/AFP/B. Stansall

Uchunguzi wa maoni ya wapiga kura , uliofanywa na kampuni ya YouGov kwa ajili ya gazeti la Times, unaonesha May anaweza kupata uungwaji mkono wa asilimia 55 ya wanachama wa chama cha Kihafidhina, akimtangulia Johnson ambae angepata asilimia 38, iwapo watu hao wawili wanaweza kufika hadi katika nafasi ya mwisho ya orodha ndogo ya wagombea wawili.

Wakati huo huo mbunge Andrea Leadsom ambaye ni maarufu katika kambi iliyofanya kampeni Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya , amesema leo kwamba huenda atagombea katika kinang'anyiro cha kuwania nafasi ya waziri mkuu David Cameron kuwa kiongozi wa chama hicho.

Uingereza na maridhiano na EU

Michael Gove mmoja kati ya viongozi waliofanya kampeni ya kijitoa kutoka Umoja wa Ulaya na waziri wa sheria ametangaza leo kwamba ataweka jina lake kuwania wadhifa wa mkuu wa chama cha Kihafidhina na hatimae kuchukua nafasi inayoachwa wazi na waziri mkuu David Cameron.

Großbritannien Boris Johnson
Boris Johnson mpiga kampeni maarufu wa "kujitoa"Picha: Reuters/M. Turner

Wakati mchakato wa kuwania madaraka katika vyama hivyo vikuu nchini Uingereza ukiendelea, taarifa zinasema kwamba Uingereza inaweza kufanya maridhiano ili kupata fursa ya soko la pamoja la Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na huenda kuchangia katika bajeti ya kundi hilo la mataifa, lakini maridhiano katika suala la uhamiaji hayana mjadala, Nigel Farage aliyefanya kampeni ya kambi ya kujitoa ameliambia gazeti la Le Figaro.

Ameongeza kwamba kufunga breki dhidi ya uhamiaji katika Umoja wa Ulaya , hicho ndio ambacho wapiga kura milioni 17.5 walituomba tufanye.

Brexit Nigel Farage
Nigel Farage kiongozi wa chama cha UK IndependencePicha: Reuters/V. Kessler

Alipoulizwa ni lini Uingereza itawasilisha ombi la kufungua kifungu cha 50 ili kuanzisha rasmi mazungumzo ya kujitoa kutoka kundi hilo la mataifa, alisema : "Naaza kufikiria kwamba hali ya sintofahamu ina gharama yake, na kwamba tunahitaji kusonga mbele na kufungua kifungu hicho cha 50 kabla ya Septemba ama Oktoba. Huenda sio kesho, lakini bila kuchelewa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe

Mhariri: Josephat Charo