1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kumshtaki Rais Musharraf wa Pakistan

Othman, Miraji8 Agosti 2008

Mpango wa kumuondosha madarakani Rais Musharraf wa Pakistan kwa kumshtaki

https://p.dw.com/p/Esqt
Pervez Musharraf akiapishwa kuwa rais wa PakistanPicha: AP

Macho ya watu yanaelekezwa leo kwa majenerali wa jeshi la Pakistan kama watamuunga mkono Rais Pervez Musharraf, ikiwa ni siku moja baada ya serekali ya mseto ya kiraia nchini humo kutangaza mpango wa kumshtaki rais huyo, ambaye zamani aliwahi kuwa mkuu wa jeshi. Bunge limeitishwa jumatatu ijayo, kukitarajiwa kutakuweko mwenendo mrefu wa malumbano juu ya hatua hiyo, ila tu ikiwa mwenyewe Perevez Musharraf atasalimu amri na kujiuzulu bila ya kutaka kun'gan'gania urais.

Bado Perevez Musharraf mwenyewe hajasema chochote hadharani kuhusu takwa lililotolewa kwake ama akabiliane na kura ya wabunge ya kutokuwa na imani naye au mwenyewe akubali ajiuzulu. Bunge limeitishwa jumatatu ijayo, siku ambapo Musharraf anatimia umri wa miaka 65. Leo umeitishwa mkutano wa majenerali katika makao makuu ya jeshi la Pakistan mjini Rawalpindi. Wachunguzi wanasema majenerali watataka kuyaangalia mambo yanakwenda vipi. Huenda wakaelezea wasiwasi wao, lakini kuelezea wasiwasi ni jambo moja na kupeleka vifaru vya kijeshi mabarabarani ni jambo lengine. Pia Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yana wasiwasi juu ya uwezekano wa nchi hiyo ya Kiislamu yenye silaha za kinyukliya na ambayo pia ni maficho ya viongozi wa mtandao wa al-Qaida kuingia katika hali mpya isiokuwa tulivu. Raia wa Pakistan hivi sasa wanashuhudia uchumi wa nchi yao ukianguka, wanakabwa na bei za vyakula na nishati zinazopanda sana. Wawekezaji katika masoko ya hisa wamepoteza asilimia 38 ya fedha zao mnamo miezi minne iliopita.

Jana Asif Zardari, mume wa waziri mkuu wa mara mbili wa Pakistan, marehemu Benazir Bhutto, na mkuu wa serekali ya mpito, pamoja na Nawaz Sharif, waziri mkuu ambaye aliondoshwa madarakani na Musharraf, walitangaza mpango wa kumshtaki rais huyo. Bwana Zardari alisema jana katika mkutano wa waandishi wa habari:

+Wananchi wa Pakistan walitoa kauli yao wazi, wakitaka demokrasia. Walipiga kura rais Musharraf aondoshwe madarakani kwa vile chama chake kimeshindwa. Na licha ya ahadi yake kwamba pindi chama chake kitashindwa yeye atajiuzulu, bado Musharraf ameganda katika wadhifa wa urais.+

Kutokana na mzozo huo, Perevez Musharraf amevunja mpango wa kwenda kushiriki katika sherehe za kufunguliwa michezo ya Olympik mjini Peking, China.

Wachunguzi wanasema rais huyo hataacha madaraka bila ya kuonesha upinzani. Inahofiwa atajaribu kulivunja bunge na kuifukuza serekali, japokuwa serekali ya mseto imesema haitalikubali jambo hilo, kama alivoweka wazi waziri mkuu wa zamani, Nawaz Sharif:

+ Nchi haitakubali kuwa na sheria za kijeshi, serekali haitabadilishwa, wala bunge halitavunjwa au jambo lolote la aina hiyo litakalofanywa na mdikteta. Jambo hilo linatambuliwa na kila mtu. Nchi yetu mara nyingi imeingiliwa na sheria za kijeshi, jeshi kujiingiza, na serekali kuondoshwa madarakani bila ya sababu. Mambo hayo yameacha majaraha makubwa. Wananchi wa Pakistan hawako tayari kujeruhiwa tena haki yao.+

Chama cha Nawaz Sharif kilisema leo baadhi ya mawaziri waliojitoa mwezi Mei kutokana na Asif Zardari kurejea nyuma katika ahadi alioitoa ya kuwarejesha mahakimu wa korti kuu makazini, watajiunga tena na serekali. Mawaziri wengine, chama hicho kilisema, watarejea punde pale majaji watakaporejeshwa makazini.

Itahitaji kura 295 kati ya 442 za mabaraza yote mawili ya bunge kuweza kumshtaki Pereve Musharraf, na inadaiwa serekali ya sasa ya mseto ina wabunge 305 upande wake.