1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kuwaondoa raia na waasi Aleppo waanza

Sylvia Mwehozi
15 Desemba 2016

Makubaliano mapya ya kusitisha amani mjini Aleppo yameanza kutumika licha ya mapigano ya usiku kucha na mabasi yamekuwa tayari kuwahamisha raia na waasi.

https://p.dw.com/p/2UIrK
Syrien Bürgerkrieg Aleppo Flüchtlinge
Picha: Reuters/A. Ismail

Mpango wa kuyahama maeneo ya waasi mjini Aleppo, Syria unaendelea hii leo licha ya mapigano yaliyoendelea usiku kucha na ulitarajiwa kuanza "ndani ya masaa", kwa mujibu wa makundi ya upinzani ya Syria na taarifa kutoka Aleppo zinasema mabasi ya kuwabeba raia wanaokimbia mji huo yalikuwa yamekaa tayari kwa ajili ya zoezi hilo.

Inakadiriwa mabasi yapatayo 20 pamoja na magari ya kuwabeba wagonjwa yamekaa tayari katika eneo la ukingo kusini mwa Aleppo yakiwasubiri wale wanaokimbia eneo hilo.

Urusi, vyanzo kutoka ndani ya jeshi na maafisa wa waasi wamethibitisha kuwa makubaliano mapya ya kusitisha mapigano yamefikiwa baada ya mpango wa awali kuvunjika jana Jumatano wakati mapigano yalipoanza.

Waasi wajisalimisha

Televisheni ya Syria imeripoti kuwa kiasi ya waasi 4000 na familia zao walikuwa tayari kuondoka. Makubaliano hayo yaliyoratibiwa na mshirika mkuu wa utawala wa Syria, Urusi na wale wanawaunga mkono upinzani, Uturuki yataweka historia ya kuhitimisha vita ya muda mrefu katika kuudhibiti mji huo wa Aleppo na ushindi kwa rais Bashar al-Assad.

Syrien Bürgerkrieg Aleppo Free Syrian Army
Askari tiifu kwa utawala wa Syria wakilinda doria katika mitaa ya waasiPicha: Reuters/G. Ourfalian

Wizara ya ulinzi mjini Moscow imesema kwamba kituo chake cha ufuatiliaji wa mpango huo kwa kushirikiana na utawala wa Syria "walikuwa wakijiandaa kuwahamisha waasi waliobaki pamoja na familia zao kutoka katika vitongoji mashariki mwa Aleppo".

Taarifa zaidi zinasema waasi huenda wamekimbia kuelekea kaskazini magharibi mwa mji wa Idlib, ambao ni ngome kubwa ya upinzani.

Al-Farook abu Bakr ambaye ni mpatanishi kwa upande wa waasi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa msafara wa kwanza utakaoondoka leo ni wale tu waliojeruhiwa  ndugu zao na raia wengine.

Hata hivyo zipo taarifa kuwa wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wameushambulia msafara wakati ukijiandaa kuondoka mapema leo na kuwajeruhi watu watatu, taarifa hizo ni kwa mujibu wa mkuu wa huduma ya dharura katika eneo hilo la mashariki mwa Aleppo.

Mpango wa awali

Mpango kama huo uliokuwa uwahamishe watu tangu jana asubuhi ulishindikana baada ya kutokea mashambulizi ya mizinga pamoja na yale ya anga. Raia waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kuondoka walilazimika kukimbilia mitaani kutafuta pa kujificha wakati mapigano yalipoanza.

Syrien Aleppo
Askari wa vikosi vya serikali wakiwa wamepumzika wakati wakiendelea kusonga mbele katika maeneo ya waasiPicha: Getty Images/AFP/G. Ourfalian

Urusi imewatuhumu waasi kwa kuvunja makubaliano hayo huku Uturuki ikishutumu utawala wa Assad na washirika wake kwa kuzuia mpango huo.

Mpango huo mpya ulitangazwa baada ya majeshi yanayoiunga mkono Syria kuanzisha mashambulizi makali ya kuuchukua tena mji wa Aleppo ambao umekuwa mikononi mwa waasi tangu 2012.

Wakiungwa mkono na majeshi yaliyopatiwa mafunzo na Iran na wapiganaji wa Kishia wa Lebanon wa harakati za Hezbollah, operesheni yao ilizidi kusonga mbele na kudhibiti karibu asilimia 90 ya maeneo ya waasi, ndani ya kipindi cha wiki nne.

Waziri wa maridhiano Ali Haider anasema kuwa "tuna lengo moja tu la kuhakikisha usalama wa raia sio wapiganaji wenye silaha. Lengo letu la mwisho ni kuhakikisha kwamba wanaweza kuondoka kwa usalama na tutafanya kila tuwezalo kuwalinda.”

Zaidi ya watu 465 wakiwemo watoto 62 wamepoteza maisha mashariki mwa Aleppo wakati wa mapigano hayo kwa mujibu wa shirika linalofuatilia haki za binadamu nchini humo.

Raia wengine 142 wakiwemo watoto 42 wameuawa na maroketi ya wasi yaliyorushwa katika ameneo yanayoshikiliwa na serikali.

Umoja wa Mtaifa na nchi za magharibi wiki hii zimelaani mauaji yanayofanywa na wapiganaji walio upande wa serikali. Umoja wa Mataifa umesema hapo jana kuwa unazo ripoti za kuwa wapiganaji waasi wanawazuia raia wanaokimbia na kuwatumia kama ngao. Zaidi ya raia laki tatu wameuawa tangu kuanza kwa mgogoro wa Syria huku mamilioni wakiyakimbia makazi yao.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters

Mhariri: Saumu Yusuf