1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa taifa wa kuwajumuisha wageni katika jamii ya Kijerumani

Maja Dreyer12 Julai 2007

Ni tukio muhimu la kihistoria – hivyo ndivyo alivyosema Kansela wa Ujerumani alipoutambulisha mpango mpya wa kuwaunganisha raia wa kigeni katika jamii ya Kijerumani. Mpango huu umeandaliwa na mashirika mbali mbali ya wahamiaji, makanisa, serikali na wengine wengi. Ila tu jumuiya nne kubwa za Kituruki zimekataa kushiriki kwenye mkutano mkubwa wa leo zikipinga sheria mpya ya uhamiaji.

https://p.dw.com/p/CB2r
Mkutano juu ya kuwajumisha wageni katika jamii
Mkutano juu ya kuwajumisha wageni katika jamiiPicha: AP

Wahamiaji Millioni 15 wanaishi Ujerumani na wote watanufaika kutokana na mpango mpya wa kitaifa wa kuwajumuisha wageni hao katika jamii. Hayo aliyasema Kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, baada ya mkutano na wajumbe wa serikali na wa jamii kuhusu suala hilo. Mpango huu ni mkusanyiko wa matokeo kutoka warsha mbali mbali zilizofanywa katika muda wa mwaka moja kati ya wajumbe hao.

Angela Merkel aliyasifu mafanikio yao: “Nnasema hilo ni tukio muhimu sana katika historia ya sera za kuwajumuisha wageni, kwani leo tumechapisha mpango wa kuwaunganisha raia wa kigeni katika jamii ambao umeandaliwa kwa pamoja na maafisa wa ngazi zote za serikali za shiriko, mikoa na mitaa pamoja na kuyahusisha makundi mbalimbali ya kijamii na vile vile wahamiaji. Ni kitu kipya kabisa ambacho hatukuwahi kuwa nacho.”

Katika mpango huo, washirika wa mkutano huu wa kitaifa wamejiwekea masharti yasiyopungua 400 yanayolenga kuwajumuisha wageni katika jamii ya Kijerumani. Tutoe mifano michache tu: Serikali imekubali kutoa fedha kuboresha hali ya elimu ya wahamiaji kwa kuwapa masomo maalum wanafunzi wenye asili ya kigeni ambao wengi wao hawaongei Kijerumani vizuri. Pamoja na jumuiya ya wafanyabiashara kuna mpango wa kuongeza nafasi za mafunzo ya kazi kwa vijana wa asili ya kigeni.

Pia serikali inazisaidia kifedha vituo vya akinamana wanaokimbia nyumbani kwa sababu walipigwa na waume zao. Serikali za mikoa zinataka kuongeza idadi ya wahamiaji wanaofanya kazi katika usimamizi. Vyombo vya habari vimekubali kuripoti zaidi juu ya masuala ya wahamiaji na mashirika kadhaa ya michezo yanataka kuwahusisha wahamiaji katika kuwafundisha vijana.

Mafanikio hayo yamechafuliwa lakini na mzozo kati ya serikali na jumuiya za watu wa asili ya Kituruki nchini Ujerumani ambazo zimekataa kushiriki kwenye mkutano wa leo.

Chanzo cha mvutano ni sheria mpya ya uhamijai. Wahamiaji wa Kituruki wanakosoa hasa kuwekwa masharti makali zaidi juu ya kumleta mke au mume aje Ujerumani. Kulingana na sheria mpya, lazime mke au mume awe ametimia umri wa miaka 18, vilevile inambidi ajifunza lugha ya Kijerumani kidogo kabla ya kufika hapa. Utaratibu huu umewekwa ili kuwarahisishia Waturuki hao kujiunganisha katika jamii ya Kijerumani.

Tukumbuke kuwa, wasichana wengi wa Kituruki wanakuja Ujerumani kuolewa kisha wanakaa majumbani au kukutana na wenzao Waturuki tu kwa sababu hawaongei lugha ya Kijerumani. Mwenyekiti wa jumuiya ya Waturuki, Bw. Kenan Kolat, ameilaani serikali ya Ujerumani kwa kuwa: “Serikali haiwezi kuwalazimisha wageni wajumuishwe wakiweka masharti fulani. Ikitaka kushirikiana nasi, lazima itusikilize ili tufanye kitu kwa pamoja.”

Jumuiya hizo za Waturuki zimemtaka rais wa shirikisho asiitie saini sheria hiyo, ama sivyo kutapelekwa shtaka mbele ya mahakama ya katiba ya Ujerumani.

Lawama hizo zimekanushwa na wanasiasa wengi wa vyama mbali mbali. Mwakilishi maalum wa serikali kwa masuala ya kuwajumuisha wageni katika jamii alisema jumuiya hizo za Kituruki zimeharibu sifa zao kwa kuukataa mwaliko huo.

Licha ya mvutano huo lakini, jumuiya za Waturuki haziuchukii mpango wenyewe na pia zinajitolea kwa kuendesha kampeni ya kuwahamasisha Waturuki juu ya umuhimu wa elimu, vilevile kuhusu haki za wanawake.