1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpasuko waibuka ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusu utoaji wa ruzuku ya kilimo

Josephat Nyiro Charo22 Septemba 2010

Ujerumani na Ufaransa zinataka mfumo unaotumika sasa kuwagawia wakulima ruzuku uendelee kutumika, huku mjadala kuhusu kuufanyia mageuzi mfumo huo, ukiendelea kupamba moto

https://p.dw.com/p/PJUO
Dacian Cioloş, kamishna wa kilimo wa Umoja wa UlayaPicha: DW/C.Stefanescu

Kumetokea mpasuko mkubwa kufuatia mkutano wa mawaziri wa kilimo wa Umoja wa Ulaya uliofanyika jana (21.09.2010) katika mji wa La Hulpe, nchini Ubelgiji kusini mwa mji mkuu, Brussels.

Huku nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zikijiandaa kupunguza bajeti zao kabla mazungumo ya bajeti ya umoja huo ya mwaka 2013, mvutano kuhusu sera ya pamoja ya kilimo unaonekana utaendelea. Waziri wa kilimo wa Ubelgiji, nchi inayoshikilia urais wa Umoja wa Ulaya, amesema kwenye mkutano wa mjini La Hulpe kwamba kuna makubaliano miongoni mwa nchi wanachama kuendeleza sera kuhusu ruzuku ya moja kwa moja kwa wakulima na kuyalinda maeneo ya mashambani.

Tatizo lakini amesema hakuna makubaliano kuhusu jinsi ya kufanya mahesabu ya ruzuku na kuzigawa kwa wakulima. Amesema haoni kuwepo kwa ari kubwa ya kufanya mageuzi ya maana. "Kila mtu amethibitisha takwa kwamba awamu hii ya kwanza isianishwe na kwamba iendelee kudhaminiwa kwa pamoja. Hata hivyo inatakiwa itilie maanani uwezo wa kukabiliana na mashindano ya kibiashara yanayotokana na kilimo, iwajali wakulima na ihakikishe mapato ya haki."

Kauli ya waziri Laurelle inaashiria mpasuko mkubwa uliopo ndani ya Umoja wa Ulaya. Nchi kadha wanachama kama vile Uingereza na Sweden zinakabiliwa na shinikizo la kupunguza kwa kiwango kikubwa ruzuku inazowapa wakulima wao. Kuna mgogoro pia kati ya nchi za Ulaya magharibi na mashariki, kati ya wanachama wa zamani wa Umoja wa Ulaya na wanachama wapya. Kwa sasa kwa mfano wakulima wa Poland hupokea kiwango kidogo cha ruzuku kuliko wakulima wa Ufaransa na Ujerumani. Kwa mantiki hiyo nchi za Ulaya mashariki zinadai nyongeza ya ruzuku. Ujerumani na Ufaransa zina msimamo wa pamoja wa kutaka mfumo unaotumika sasa uendelee kutumika.

Bila shaka matatizo ya sera za kilimo za Umoja wa Ulaya hazihusiani na ukubwa wa nchi wanachama na umuhmu wa kilimo. Kamishna wa kilimo katika Umoja wa Ulaya, Dacian Ciolos, ameelezea wasiwasi wake kwamba idadi ya vijana wanaotaka kuwa wakulima katika siku za usoni inazidi kupungua kwa kasi kubwa.

"Ni muhimu kutilia maanani masilahi ya vijana ili waweze pia kushiriki katika shughuli za kilimo. Sitaki nichukue hatua ya hatari kwamba tunagombana kuhusu sera ya pamoja ya kilimo na kisha baada ya miaka kadhaa kuwe hakuna wakulima tena, tutakaowahitaji kutekeleza sera hizi mpya za kilimo."

Hata msaada kwa wakulima vijana kila mara unahusiana na fedha. Malumbano ya wazi kuhusu ruzuku ya kilimo bado hayajaanza barabara. Waziri wa kilimo wa Ujerumani, Ilse Aigner, amebashiri kuwa mivutano kuhusu ruzuku ya kilimo itakuwa vita vya kusisimua.

Mwandishi: Hasselbach, Christoph (DW Brüssel) /Josephat Charo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman