1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

050810 Campbell Taylor Blutdiamanten

Sekione Kitojo5 Agosti 2010

Kwa muda wa miaka 11, hadi mwaka 2002 vilizuka nchini Sierra Leone vita vya wenyewe kwa wenyewe, sababu ya vita hivyo kuchukua muda mrefu ni biashara haramu ya madini ya almasi.

https://p.dw.com/p/OcTM
Mrembo wa kuonyesha mavazi raia wa Uingereza Naomi Campbell ametoa ushahidi hii leo katika kesi inayomuhusisha dikteta wa zamani wa Liberia Charles Taylor kuhusu zawadi aliyopewa ya almasi katika mahakama ya kimataifa mjini The Hague.Picha: AP

Kwa  muda  wa  miaka 11 , hadi  mwaka  2002, vilizuka nchini  Sierra  Leone  vita vya   wenyewe  kwa  wenyewe . Sababu  iliyofanya   vita  hivyo  kuchukua  muda  mrefu kiasi  hicho , ni  biashara  ya  almasi   ambayo  ilikuwa ikitumiwa   kugharamia   makundi  ya  waasi. Charles Taylor  alikuwa  wakati  huo  rais  wa  nchi  jirani  ya Liberia.  Ameshiriki  katika  biashara  hii  ya  almasi  na kusaidia  kuendeleza  vita  hivyo  vya  wenyewe  kwa wenyewe. Anashtakiwa  kwa  hiyo  kwa  mauaji, kuwaandikisha  watoto  jeshini, kusababisha  ulemavu,  na uporaji , katika  mahakama  maalum    kuhusu  Sierra Leone  katika  mji  wa  The  Hague  nchini  Uholanzi.Taylor amekana  mashtaka  hayo . Mahakama  hiyo  imekuwa  na wasi  wasi  hata  hivyo  kutokana  na   shahidi  wake  huyo anayefahamika  sana.

Siku  moja  katika  mwaka  1997, mrembo  huyo  wa kuonyesha  mavazi  ambaye  ni  maarufu  duniani   Naomi Campbell  alihudhuria    hafla  iliyoandaliwa  na   rais  wa zamani  wa  Afrika  kusini  Nelson  Mandela.  Katika  hafla hiyo  alikutana  pia  na   kiongozi  huyo  wa  zamani  wa Liberia Charles  Taylor. Taylor  alivutiwa  sana   na  uzuri wa  Naomi ambapo  baada  ya  hafla  hiyo  alimzawadia almasi  ambazo  hazijakatwa  katika  chumba  chake  cha hoteli  alimofikia. Leo  hata  hivyo  anaonna   na  mtu  huyo aliyemhusudu  lakini  mara   hii  akiwa  kizimbani  katika mahakama  hiyo  na  anatakiwa  kutoa  ushahidi  dhidi yake.

Kesi  hiyo  ambayo  ilianza   kwa  mara  ya  kwanza Januari  2008, ni  ya  kwanza  kwa   rais  aliyekuwa akitawala   barani  Afrika  ameweza  kufikishwa mahakamani. Ni  kesi  inayofungua  njia, kama  Elly Harrowell  kutoka  katika  shirika  la  kutetea  haki  za binadamu   nchini  Uingereza , Global  Witness anavyoelezea.

Aina  hii  ya   kesi  inatoa  ishara  ya  wazi, kuwa  yule ambaye  atafanya  uhalifu  mkubwa   dhidi  ya   binadamu , atafikishwa  katika  mkono  wa  sheria. Na  Charles  Taylor atawajibishwa  kwa   kile  alichokifanya.

Mrembo  huyo  wa  kuonyesha  mavazi  Naomi  Campbell amewaambia  waendesha  mashtaka  katika  mahakama ya  kimataifa   kuwa  alipewa   almasi  hizo  kama  zawadi nchini  Afrika  kusini  mwaka  1997, lakini  hakufahamu iwapo  madini  hayo  ambayo  yalikuwa  machafu yalitolewa  na  rais  wa  zamani  wa  Liberia  dikteta Charles  Taylor.

Amesema   kuwa  almasi  hizo   alipewa  zikiwa  katika kisanduku  cha  vito  katika  hoteli  alimofikizia  na  watu wawili, lakini  akaongeza  kuwa   hakuuliza kisanduku hicho  kinatoka  kwa  nani.

Alifungua  kisanduku  hicho  siku  ya  pili, anasema. Aliona mawe  machache. Yalikuwa  madogo   na   yalionekana machafu.

Mrembo  huyo amesema  kuwa  aliambiwa  wakati  wa kifungua  kinywa  asubuhi  na  mcheza  sinema  kutoka Marekani  Mia Farrow  pamoja  na  mshauri  wake  wa masuala  ya  mahusiano  kuwa  mawe  hayo  huenda  ni  ni almasi  ambazo  hazijakatwa  ambazo  huenda  zimetumwa na  Charles Taylor.

Mwendesha  mashtaka   wa  mahakama  hiyo Brenda Hollis  amesema   kuwa  anamatumaini  ya  kuthibitisha kutokana  na   kauli  ya  Campbell    kuwa  dikteta  huyo wa  zamani  wa  Liberia  alikuwa  na  kile  kinachoitwa almasi  za  damu, zilizopatikana   kutoka  katika  maeneo ya  waasi  ili  kugharamia   ununuzi  wa  silaha  za mamilioni  ya  dola  kwa   ajili  ya  Sierra  Leone.

Mwandishi : Shale, Andrew / ZR /  Sekione  Kitojo

Mhariri : Mohammed  Abdul Rahman

E N D E