1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wauwa 71 Abuja

Mohamed Dahman14 Aprili 2014

Mripuko wa bomu wakati wa harakati za asubuhi kwenye kituo cha basi katika kiunga cha mji mkuu wa Nigeria Abuja umeuwa takriban watu 71 Jumatatu (14.04.2014) na kuzusha wasi wasi juu ya kuenea kwa uasi wa Boko Haram.

https://p.dw.com/p/1Bhrp
Hali ya taharuki kufuatia mripuko katika kituo cha basi katika kiunga cha Abuja,Nigeria. (14.04.2014)
Hali ya taharuki kufuatia mripuko katika kituo cha basi katika kiunga cha Abuja,Nigeria. (14.04.2014)Picha: picture alliance/AP Photo

Tuhuma zinaelekezwa dhidi ya kundi la Boko Haram juu ya kwamba hakuna taarifa ya kudai kuhusika na shambulio hilo kutoka kwa wapiganaji hao wa itikadi kali za Kiislamu ambapo hasa wamekuwa wakiendesha zaidi harakati zao kaskazini mashariki mwa Nigeria.Mbali ya watu 71 waliouwawa polisi imesema watu 124 wamejeruhiwa katika shambulio hilo ambalo ni la kwanza kufanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo katika kipindi cha miaka miwili.

Kamadori wa kikosi cha anga Charles Otengbade ambaye ni mkurugenzi wa oporesheni za msako na uokozi amesema wataalamu wa usalama wanashuku kwamba bomu hilo limeripuka likiwa ndani ya basi.

Mabaki ya maiti za watu zilizorowa damu ilikuwa imetapakaa kila mahala wakati vikosi vya usalama vikihangaika kudhibiti umma wa watu uliokuwa umezonga kutaka kujuwa kilichojiri na askari wa zima moto wakilimwagia maji basi ambalo bado lilikuwa na miili ya abria ilitoketea.

Rais Jonathan aapa kuwashinda Boko Haram

Shambulio hilo linaonyesha jinsi ilivyo rahisi kwa mji huo mkuu wa Nigeria kuweza kushambuliwa ambao umejengwa katika miaka ya 1980 kwa kuzingatia umbo la kijiografia ya nchi kuchukuwa nafasi ya mji wa Lagos kama makao makuu ya serikali katika nchi hiyo ambayo hivi sasa ndio yenye nguvu kubwa kabisa za kiuchumi barani Afrika na mzalishaji mkuu wa mafuta.

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ameapa kwamba nchi hiyo itaushinda uasi huo wa kinyama wa kundi la Boko Haram wakati akitembelea eneo kulikotokea mripuko huo katika kituo cha basi.

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria.
Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria.Picha: picture alliance / dpa

Jonathan akizungumuza kwenye kituo hicho cha basi cha Nyanya kilioko kwenye viunga vya mji mkuu wa Abuja amesema wamepoteza watu kadhaa na kwamba suala hilo la Boko Haram ni historia mbaya kabisa inayotokea ndani ya kipindi cha maendeleo ya nchi hiyo lakini watawashinda Boko Haram na kwamba suala hilo ni la mpito.

Kuongezeka mashambulizi

Wanamgambo wa Boko Haram wanopigania kuanzishwa kwa taifa la Kiislamu wamejikita zaidi katika eneo la mbali la kaskazini mashariki ambapo wamekuwa wakiendesha harakati zao katika kipindi cha miezi kadhaa iliopita na wamekuwa wakizidi kuwalenga raia katika mashambulizi yao ambao wanawatuhumu kwa kutowa ushirikiano wao kwa serikali na vikosi vya usalama.

Hali kufuatia mripuko kwenye kituo cha basi katika kiunga cha Abuja. (14.04.2014).
Hali kufuatia mripuko kwenye kituo cha basi katika kiunga cha Abuja. (14.04.2014).Picha: Reuters

Meja Yahya Shinku afisa wa zamani katika jeshi la Nigeria anazungumzia kwa nini mashambulizi hayo yamekuwa yakizagaa kutoka nje ya eneo la kaskazini mashariki. Amesema "Baadhi ya mashambulio haya yamechochewa kisiasa na hayawezi kutenganishwa na ukweli kwamba tunaelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo kuna watu wana maslahi yao.

Baadhi ya watu wanaona shambulio hilo sio la kushangaza kwani hali ilikuwa ikizidi kuwa mbaya na huo ni kama ujumbe kwamba kundi hilo la Boko Haram bado lingalipo na linaweza kushambulia Abuja wakati wanapotaka na kusababisha hofu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman