1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mrithi wa Cameron nani na lini?

26 Juni 2016

Uamuzi wa waziri mkuu wa Uingereza David Cameron kujiuzulu baada ya kushindwa katika kampeni ya kuibakisha Uingereza katika Umoja wa Ulaya umezusha mchuano wa kuwania wadhifa huo katika chama cha Conservative.

https://p.dw.com/p/1JDn0
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron
Picha: picture-alliance/abaca

Mchakato umeshanza wa kumtafuta mrithi wake na mshindi atachukua nafasi yake katika mtaa wa Downing namba 10. Tayari Cameron amekwisha sema kwamba atajiuzulu kabla ya uchaguzi ujao mwaka 2020, na wabunge kadhaa wa chama cha Conservative wamejiweka tayari kuwa warithi wake.

Waziri mkuu ajaye wa Uingereza atakuwa na jukumu la kufanya majadiliano ya kuitoa nchi hiyo kutoka Umoja wa Ulaya.

Hizi ndio hatua muhimu zinazofuatia kujiuzulu kwake: Cameron aliitisha kura ya maoni na kufanya kampeni kwa nguvu zote ya "kubakia" katika kura ya maoni iliyofanyika siku ya Alhamis, kwa hiyo kuondoka kwake kulikuwa hakuzuiliki, lakini ni mwisho wenye kudhalilisha katika muda wake wa kazi.

Cameron mwenye umri wa miaka 49 alikuwa waziri mkuu mwenye umri mdogo kabisa nchini Uingereza mwaka 2010 , katika muda wa miaka 200 iliyopita, na mwaka jana alichaguliwa tena kwa wingi mkubwa wa chama cha Conservative.

Boris Johnson meya wa zamani wa London
Boris Johnson meya wa zamani wa LondonPicha: Getty Images/AFP/L. Neal

Cameron atakabidhi uongozi na funguo ya nyumba ya mtaa wa Downing utakapofanyika mkutano wa chama hicho mwezi Oktoba.

Anakiacha chama kikiwa kimegawanyika mno, ambapo sita kati ya mawaziri wake na wabunge 128 kati ya wabunge 330 wa chama chake cha kihafidhina wakiwa wameunga mkono kujitoa.

Kamati ya wabunge waandamizi

Kamati ya wabunge waandamizi wa chama hicho cha kihafidhina watakutana Jumatatu kuanza rasmi mchakato wa kumpata kiongozi.

Watu wanaotarajiwa kuwania wadhifa huo ni hawa.

Boris Johnson, ambaye aliongoza kampeni ya kujitoa, ndie aliyetia nguvu zaidi kampeni ya kujitoa. Meya huyo wa zamani wa mji wa London mwenye umri wa miaka 52 amejijengea umaarufu kwa watu wengi wenye shaka na Umoja wa Ulaya miongoni mwa wapiga kura wa chama cha Conservative.

Michael Gove: Ni waziri wa sheria na rafiki mkubwa wa David Cameron na uamuzi wake wa kumkana na kufanya kampeni ya kujitoa ilikuwa ni pigo kwa waziri mkuu.

Theresa May, ni waziri wa mambo ya ndani na aliepuka vita vya ndani ambavyo viligubika kampeni hiyo, na hatua hiyo inampa nafasi adimu kuwa mmoja kati ya wale wanaoweza kumrithi Cameron.

Theresa May waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza
Theresa May waziri wa mambo ya ndani wa UingerezaPicha: picture-alliance/empics/J. Brady

George Osborne, ni waziri wa fedha ,na mshirika wa karibu wa Cameron , na amekuwa kwa muda mrefu akitajwa kuwa na uwezekano wa kumrithi waziri mkuu, lakini uungaji wake mkono kura ya "kubakia" umewakasirisha wengi wa wapiga kura wa chama hicho.

Merkel atuliza mzuka

Wengine wanaoangaliwa kuwa na uwezekano wa kumrithi Cameron ni pamoja na mawaziri wawili wanaopendelea Umoja wa Ulaya , Nicky Morgan, waziri wa elimu na Stephen Crabb, waziri wa kazi na mafao ya uzeeni.

Nchini Uingereza wapiga kura wanakichagua chama na sio waziri mkuu, kwa hiyo mabadiliko ya juu ya uongozi hayahitaji kuitishwa uchaguzi mpya.

Wakati huo huo kansela wa Ujerumani Angela Merkel alijaribu jana Jumamosi (25.06.2016) kupunguza mbinyo kutoka Paris, Brussels na serikali yake kuilazimisha Uingereza kuingia katika mazungumzo haraka ya kuvunja ndoa kati ya Umoja wa ulaya na Uingereza, licha ya onyo kwamba kusitasita kutasababisha hisia za kizalendo kuota mizizi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga