1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MSAADA KWA OPEL?

18 Novemba 2008

Msaada kwa viwanda vya magari kutokana na msukosuko wa uchumi.

https://p.dw.com/p/FxUE

Serikali ya Ujerumani imejitolea kukichukulia dhamana kiwanda cha magari cha Opel kwa kitita cha mabilioni ya fedha. Baada ya mazungumzo na mwenyekiti wa Bodi ya General Motors-Tawi la Ulaya Carl-Peter Forster,mwenyekiti wa bodi ya Opel nchini Ujerumani Hans Demant pamoja na mwenyekiti wa Halmashauri ya Opel Klaus Franz,Kanzela Angela Merkel ametangaza kuwa serikali ya Ujerumani,itaamua kabla X-masi juu ya ombi OPEL la msaada huo.

Tofauti na waziri mkuu wa jimbo la Hesse Roland Koch ambae akiitikia mwito huo wa dharura kutoka Opel kuwa ni ngao ya kuyalinda makampuni yote ya motokaa ya Ujerumani na alikuwa tayari kuchangia Euro milioni 500 kutoka hazina ya serikali yake ya mkoa,viongozi wa juu wa serikali ya Ujerumani mjini Berlin, wameanza tu kuikagua hali ya mambo ilivyo ya kiwanda hiki cha magari.Na hatua hii yafaa kukaribishwa kwani, tawi hili la kiwanda cha motokaa cha Marekani- General motors ,hakijaingia hatarini sana kufilisika.Na hata kwa jicho la kutopendelea kampuni lolote kwa kulipa nafuu zaidi za kibiashara pale serikali inapolisaidia kampuni moja na kuacha jengine, ambalo kwa sababu zozote zile limeingia hatarini kufilisika.

Uongozi na Baraza la kiwanda cha tawi la GM- Opel limeitaka serikali ya shirikisho huko Berlin na za mikoa kuwa zisaidie viwanda vya motokaa vya Opel endapo vikiomba msaada.Endapo kiwanda mama cha GM nchini Marekani kimetangaza kufilisika kiipe Opel mkopo ambao hautatumiwa na kiwanda kikuu cha Marekani.Bado hizo ni hofu tu hali haijafikia hapo,kwani nchini Marekani kwenyewe kunaandaliwa mpango wa kitita cha dala bilioni 25 ili kuviokoa viwanda 3 vikuu vya motokaa humo nchini -GM,Ford na Chrysler.

Ni busara kuizingatia kwanza hali ya mambo kuliko kukurupuka na kuchukua hatua za haraka-haraka.

Kwa mfano, haina maana fedha za walipakodi wa Ujerumani kutumika ikiwa kuna hatari kwamba zitakinufaisha kiwanda kikuu nchini Marekani.

Kufuatia mazungumzo yaliofanyika jana katika afisi ya Kanzela huko Berlin,ilidhihirika wazi: serikali kuu ya shirikisho na zile za mikoa ambako kuna matawi ya kiwanda cha Opel,hakitaachiwa kuanguka.

Lakini moja ni wazi hakutatolewa dhamana ya kusaidia kifedha bila masharti: Wala serikali ya Ujerumani huko berlin na za mikoani hazitavitia jeki viwanda vyote vya motokaa humu nchini.Viwanda vyengine mfano wa Daimler,BMW,VW na Porsche,viko katika hali njema kufuatia miaka minono ya biashara .Viwanda hivyo havipepesuki na wala havina kasoro ya fedha bali vina kasoro tu ya wanunuzi wa magari yao.

Lakini licha ya msaada wa serikali na kutiwa jeki, magari yanayokula mafuta na gesi nyingi ya viwanda hivi vikubwa, hayatavikomboa kabisa kutoka msukosuko wa sasa. Kuchukuliwa ama dhamana au kupewa msaada wa mikopo hakutatosha na wala mradi wa kustawisha uchumi unaodorora.

Kwani, wanunuzi wa magari hawataki tena magari ya aina hiyo yanayokula petroli.Viwanda vya magari hapo vinapaswa kujirekebisha.Kuunda aina mpya ya motokaa zitakazolingana na mahitaji ya sasa ya wanunuzi magari,kutachukua muda na kugharimu fedha.Na katika kesi nyengine mbaya hata kuongoza kufilisika kwa baadhi ya viwanda vya magari na nafasi za kibarua.

Jambo moja pia ni wazi,viwanda vya magari ni muhimu kiuchumi lakini sio nguzo muhimu sana kiuchumi kama Mabenki yalivyo.Hatahivyo, serikali haitafumba tu mikono bila kusaidia viwanda vinavyoweza kufilisika.

Katika kampuni la Opel nchini Ujerumani, nafasi za kazi 25.000 ziko hatarini na nyengine 50.000 kwa viwanda vidovidogo vinavyovipatia viwanda hivyo vikubwa vipuri vyao.