1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msafara wa treni ya Castor wakurubia kufika ufundoni

Oumilkher Hamidou8 Novemba 2010

Maandamano ya wapinzani wa nishati ya kinuklea wakorofisha msafara wa treni iliyosheheni takataka za kinuklea

https://p.dw.com/p/Q1R2
Maandamano dhidi ya safari ya treni CastorPicha: dapd

Machafuko yaliyosababishwa na msafara wa treni ya Castor iliyosheheni takataka za kinyuklia zinazorejeshwa Ujerumani baada ya kusafishwa katika mji wa La Hague nchini Ufaransa, ndio mada iliyohanikiza magazetini hii leo.

Gazeti la "DARMSTÄDTER ECHO "linaandika"Sio lazima mtu awe mtume kuweza kutambua kwamba maandamano ya Wendland dhidi ya msafara wa treni ya Castor yamejipatia kipeo cha aina mpya: makubwa, yamepanuliwa na yanawaleta pamoja watu wengi-lakini pia yanaonyesha kushawishiwa na matumizi ya nguvu. Serikali kuu ya muungano kutoka vyama ndugu vya CDU/CSU na waliberali wa FDP imechangia sana katika hali hiyo. Kwa kupitisha uamuzi wa kurefusha muda wa vinu vya nishati ya kinyuklia, serikali ya muungano imefufua vuguvugu la wapinzani wa nishati ya kinyuklia ambalo tayari lilikuwa limeshasahauliwa.

Gazeti la Kaskazini mwa Ujerumani,"Kieler Nachrichten" linaandika:"Washirika wa serikali kuu ya muungano toka vyama ndugu vya CDU/CSU na waliberali wa FDP,wanawaachia uwanja upande wa upinzani. Badala ya kuelezea umuhimu wa kuwepo bohari ya takataka za kinyuklia, badala ya kusaka namna ya kubuni nishati ya kinuklea isiyochafua hali ya hewa, badala ya sheria kwendewa kinyume huko Wendland, wanawasukumizia dhamana polisi. Watu kwa hivyo wasishangae kuwaona waandamanaji wanadhibiti hoja za nguvu na uchokozi. Wanaweza kujinata kuwa wao ndio wababe waliofanikiwa kuuzuia msafara wa treni ya Castor. Hakuna kweli aliyejiuliza kwa nini msafara wa treni ya Castor unaoelekea Gorleben ni hatari ikiwa kabla ya hapo uliweza kuzuiliwa kwa siku nzima bila ya kuhofia hatari ya aina yoyote inayoweza kutokea?

Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" la mjini Karlsruhe linahisi:"Msafara wa Castor ni kisingizio tuu cha watu kuteremka majiani. Sababu halisi zinatokana na ile hali ya watu kutojua la kufanya, ukosefu wa imani na bumbuwazi kati ya watawala na wanaotawaliwa. Asilimia 61 ya wananchi wa Ujerumani wanapinga sera ya nuklea ya serikali ya muungano wa nyeusi na manjano,wengi wa wananchi wanaamini Merkel na wenzake wanatumikia masilahi ya makampuni ya nishati ya kinuklea. Lakini badala ya kutilia maanani hofu za wananchi, kuwaelezea umuhimu wa sera yao ya nishati na kuwataka wawaelewe na kuwaamini, kansela na waziri wa mazingira wanayakosoa maandamano, wakisema sera yao haina mbadala na kwa namna hiyo kuzidisha hali ya kutoaminiana."

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mpitiaji: Josephat Charo