1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alitaka kujiua?

26 Machi 2015

Andreas Lubitz, msaidizi wa rubani wa ndege ya Germanwings ambaye vyombo vya sheria vya Ufaransa vinamtuhumu kuiangusha makusudi ndege hiyo katika milima ya Alpes alikuwa kijana wa kawaida tu.

https://p.dw.com/p/1Ey5t
Chumba cha rubani cha ndege ya Germanwings iliyoangushwa na Andreas LubitzPicha: Reuters/L. Foeger

Huko Montabaur,mji mdogo wa wakaazi 12 elfu, alikokuwa akiishi, umbali wa kilomita 20 kaskazini mashariki ya mji wa Coblence, wakaazi wameduwaa, wamepigwa na mshangao.

"Alikuwa kijana wa kawaida kabisa" amesema Klaus Radke,anaeongoza kilabu ya shughuli za usafiri wa ndege ambako Lubitz ndiko alikopata liseni yake ya kwanza ya kuendesha ndege,miaka kadhaa iliyopita.

Msimu wa mapukutiko mwaka jana,kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 alirejea huko huko ili kuendelea na mafunzo ya kuendesha ndege pamoja na mwalimu Klaus Radke.

"Alikuwa kijana mpole,mcheshi na adabii" ameongeza kusema Klaus Radke.

Andreas Lubitz hakuwa na maingiliano yoyote na kundi la kigaidi-amehakikisha kwa upande wake waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas de Maizière.

Deutschland Schild des Fliegervereins des Germanwings Ko-Piloten Andreas Lubitz
Kilabu cha shughuli za Safari za ndege alikosomea kwanza Andreas LubitzPicha: AFP/Getty Images/P. Stollarz

Maisha yake yalikuwa mazuri,alikuwa anashiriki katika mashindano ya mbio fupi za marathon ,akipenda muziki wa pop na akipenda pia kwenda kwenye vilabu vya usiku-kwa mujibu wa ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Facebook wenye picha yake,akisimama mbele ya daraja ya Golden Gate huko San Francisco.

"Sina la kusema...nnashindwa kuelewa"kutokana na kumjua Andreas,nashindwa kuamini" amesema Peter Rücker ambae ni mwanachama wa kilabu ya shughuli za safari za ndege.

"Andreas alikuwa kijana mwenye haiba,mtu anaependa sana kufanya maskhara,hata kama baadhi ya wakati alikuwa kimya.Alikuwa kama vijana wote wengine wanaoishi huku."

"Alikuwa na marafiki wengi,hakuwa mpweke,alikuwa sehemu kamili ya kundi hili" ameongeza kusema Rücker.

Karibu na nyumba ndogo ya rangi nyeupe alikokuwa akiishi Lubitz,jirani yake Hans-Jürgen Krause anasema "ameshangazwa kupita kiasi."

Kila aliyekuwa akimjua ameduwaa

Armin Pleiss,mkuu wa shule ya sekondari ya Mons-Tabor,alikosomea kijana huyo,nae pia anasema ameshangaa na kupigwa na bumbuwazi sawa na watu wote wengine.

Deutschland PK zum Absturz Germanwings A320 Köln/Bonn
Mkutano na waandishi habari uliofanywa na uongozi wa Germanwings mjini ColognePicha: Reuters/W. Rattay

Germanwings,tawi la safari za bei nafuu za shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa imesema Lubitz ana jumla ya masaa 630 tangu alipoanza kazi ya rubani katika wakati ambapo kamanda alikuwa na zaidi ya saa 6000 baada ya kufanya kazi kwa muda wa miaka 10 na shirika hilo la ndege la Ujerumani.

Lubitz amepata mafunzo ya urubani katika shule ya Lufthansa mjini Bremen.

Mwenyekiti wa baraza la uongozi la shirika la Lufthansa,Carsten Spohr amesema kijana huyo alichukua likizo ya miezi kadhaa baada ya mafunzo yake yaliyodumu miaka sita.Ameongeza kusema lakini hilo si jambo geni miongoni mwa marubani wanafunzi kutokana na ugumu wa mafunzo hayo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri:Josephat Charo