1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msako nyumba kwa nyumba Gambia

3 Januari 2015

Majeshi ya usalama ya Gambia katika mji mkuu Banjul Ijumaa(02.01.2015)yamekuwa yakiingia nyumba hadi nyumba kuwasaka waliohusika katika jaribio lililoshindwa la mapinduzi dhidi ya kiongozi wa nchi hiyo Yahya Jammeh.

https://p.dw.com/p/1EESB
Yahya Jammeh 2006
Wanajeshi wa kikosi cha ulinzi wa rais GambiaPicha: picture-alliance/AP/Rebecca Blackwell

Watu walioshuhudia wamesema vikosi vya jeshi la nchi hiyo , ambavyo pia vimeweka vituo vya upekuzi katika barabara inayoelekea nje ya mji huo wa pwani, walikuwa na wanawatafuta watuhumiwa wa shambulio la Jumanne katika makaazi ya rais.

Shambulio hilo, ambalo lilirudishwa nyuma na majeshi ya ulinzi, lilitokea wakati Jammeh alikuwa katika ziara ya binafsi nchini Dubai, duru za kidiplomasia na jeshi nchini humo zimesema.

Yahya Jammeh 02/2014
Rais Yahya Jammeh wa GambiaPicha: picture-alliance/AP/Sunday Alamba

Msako wa nyumba kwa nyumba

"Wanajeshi wa Gambia wakiwa na silaha wanafanya msako wa nyumba kwa nyumba," mwanamke mmoja anayeishi mjini Banjul ameliambia shirika la habari la AFP, akiomba kutotajwa jina. "Wanaamini washambuliaji hao bado wamejificha katika mji mkuu huo."

Wakaazi katika vitongoji vingine pia wameripoti nyumba kupekuliwa.

Mvuvi mmoja , pia ameomba asitajwe jina lake kwasababu ya hali ya hofu katika mji huo, amesema ameonywa na ndugu zake kutorudi nyumbani akiwa na samaki aliowavua katika eneo la kawaida la kufunga gati nje ya mji wa Banjul kwasababu "wanajeshi wametega kuvamia kwa kushitukiza katika maeneo ya miinuko katika daraja la Denton na Old Jeshwang".

Karte Gambia mit Hauptstadt Banjul und Guinea-Bissau
Ramani ya Gambia

Maafisa wa jeshi na serikali hawakupatikana kutoa maelezo.

Duru katika idara ya upelelezi imesema siku ya Alhamis kwamba watu kadhaa wamekamatwa kwa kuhusika na shambulio hilo la alfajiri, ambalo lilifanywa na watu wenye silaha nzito waliokuwa wakisafiri kwa boti.

Duru za jeshi la Gambia zimesema jaribio hilo la mapinduzi liliongozwa na mwanajeshi mwenye cheo cha kapteni aliyeasi jeshi na ameuwawa pamoja na washambuliaji wengine wawili.

Watuhumiwa wengine wanne walioshiriki katika jaribio hilo wamekimbilia katika nchi jirani ya Guinea-Bissau , imesema duru kutoka katika jeshi la nchi hiyo kuliambia shirika la habari la AFP.

Ukiukaji wa haki za binadamu

Jammeh , mwenye umri wa miaka 49, ambaye binafsi aliingia madarakani katika mapinduzi , ameliongoza taifa hilo dogo la Afrika magharibi ambalo liko sambamba na mto Gambia kwa miaka 20.

Urais wake umegubikwa na shutuma za ukiukaji wa haki za binadamu na wadadisi wameonya kuwa shambulio la Jumanne linaweza kutumiwa kama sababu ya kuhalalisha ukandamizaji.

Siku ya Alhamis ameshutumu vikosi vya nje ambavyo havikutambulika kwa kujaribi kumuondoa madarakani na amesisitiza kwa jeshi lake ni "tiifu mno kwake".

"Haya hayakuwa mapinduzi. Hili lilikuwa shambulio lililofanywa na kundi la kigaidi likiungwa mkono na baadhi ya mataifa makubwa ambayo sitaki kuyataja," amesema.

Gambia Straßenszene in Banjul
Mji wa Banjul , hofu imetanda wakati huu wa msakoPicha: picture-alliance/maxppp/M. Aliou

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika mataifa ya Afrika Magharibi , Mohammed Ibn Chambas , ameshutumu " jaribio la kukamata madaraka kwa njia ambazo ni kinyume na katiba".

Ibn Chambas , ambaye anatarajiwa kuizuru Gambia hivi karibuni, ametoa wito kwa majeshi ya ulinzi "kuhakikisha kwamba uchunguzi unafanyika kwa kuheshimu haki za binadamu na hatua za kawaida za kisheria".

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Abubakar