1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msako wafanywa kufuatia mashambulizi ya Munich

23 Julai 2016

Polisi wanatafuta taarifa kufahamu kwa nini kijana wa umri wa miaka 18 raia wa Ujerumani mwenye asili ya Iran aliushambulia kwa risasi umati wa watu katika jumba la maduka la Olympia na mgahawa wa chakula mjini Munich.

https://p.dw.com/p/1JUk3
Deutschland Tödliche Schießerei in München
Picha: Reuters/M. Dalder

Mashambulizi ya mjini Munich yamesababisha operesheni kubwa ya polisi wakati ambapo maafisa walikabiliwa na kishindo cha mashambulizi ya Würzburg na Nice nchini Ufaransa. Polisi wanakusanya taarifa kutoka kwa watu walioshuhudia mashambulizi ya jana yaliyofanywa na washambuliaji waliokuwa wamejihami na bunduki muda mfupi kabla saa kumi na mbili jioni saa za Ujerumani. Mshambuliaji huyo aliwaua watu tisa kabla kujiua mwenyewe. Watu wengine 16 walijeruhiwa katika mashambulizi hayo.

Msemaji wa polisi ya Munich, Peter Beck, amesema maafisa bado wanaendelea na kibarua kigumu cha kukusanya ushahidi katika eneo la tukio. Hata hivyo amekataa kuthibitisha ripoti za gazeti la Ujerumani, Bild, kwamba maafisa wamevamia makaazi katika mji wa Marxvorstadt takriban kilometa mbili kutoka kwa jengo la maduka la Olympia na kwamba walikuwa wakimohiji baba wa mshukiwa, akisema uchunguzi ungali unaendelea.

Polisi wamesema watu watano kati ya kumi waliokufa walikuwa na umri wa chini ya miaka 18, bila kutoa taarifa za kina. Wengine waliouliwa walikuwa watu wazima.

Deutschland Olympia Einkaufszentrum in München Polizei NEU
Polisi wakipiga doria eneo la maduka la OlympiaPicha: Getty Images/AFP/C. Stache

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajiwa leo kuongoza kikao cha dharura cha baraza la usalama la mawaziri. Waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere ameamuru bendera zipeperushwe nusu mlingoti, kuonyesha huruma kufuatia tukio hilo la kinyama. De Maiziere atakutana na wakuu wa idara za usalama mjini Berlin kabla kujiunga na mawaziri wengine wa ngazi ya juu kwa mazungumzo ya baraza la usalama, mwenyekiti akiwa kansela Merkel.

Mshirika wa karibu wa kansela Merkel, Volker Kauder, ameitolewa wito Ujermani ichukue hatua kukomesha kuenea machafuko kufuatia mashambulio ya Munich. Kauder, ambaye ni kiongozi wa chama cha kihafidhina cha kansela Merkel cha Christian Democratic Union, CDU, katika bunge la Ujerumani, Bendestag, amesema pana haja ya kuhakikisha chuki na machafuko katika jamii havienei zaidi.

Mashambulizi yalaaniwa

Rais wa Marekani Barack Obama amelaani mashambulizi ya Munich. "Bila shaka tunawatakia kheri wale wote ambao huenda wamejeruhiwa. Ni hali ambayo bado ni tete. Ujerumani ni mojawapo ya nchi washirika wetu wa karibu kwa hiyo tunaahidi kutoa msaada wote ambao huenda ukahitajika katika kushughulikia na kuyakabili mashambulizi haya."

Iran imelaani vikali mashambulio ya Munich na kuuleza ugaidi kuwa aibu ya nyakati za sasa, lakini ikajiepusha kusema chochote kuhusu mshukiwa. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Bahran Ghasemi, amesema, "Tunaomboleza na Wajerumani na serikali na tunalaani matukio ya mjini Munich."

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ametuma risala za rambirambi kwa kansela Merkel na waziri mkuu wa Bavaria, Horst Seehofer, kufuatia mashambulizi ya risasi ya Munich.

Mwandishi:Josephat Charo/reuters,afp,ap

Mhariri:Mohammed Dahman