1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliopeteza ndugu watoa msamaha kwa mtuhumiwa

20 Juni 2015

Ndugu na jamaa za watu waliouawa katika kanisa la mji wa Charlestone wametoa msamaha kwa mtuhumiwa wa mauaji, lakini pia wameyatoa machungu yao.Hata hivyo Gavana wa jimbo la South Carolina ataka adhabu ya kifo

https://p.dw.com/p/1Fk4W
Mtuhumiwa wa mauaji Dylann Roof
Mtuhumiwa wa mauaji Dylann RoofPicha: Reuters/Pool TPX Images of the day

Ndugu na jamaa za watu tisa waliouliwa kwa kupigwa risasi kanisani, jana walimkabili mtuhumiwa wa mauaji, Dylann Storm Roof mahakamani lakini bila ya kuonana naye ana kwa ana. Ndugu na jamaa hao waliyaelezea machungu, ghadhabu, lakini pia upendo wao kwa njia ya video. Dylann Roof anatuhumiwa kuwaua watu hao tisa ndani ya kanisa kongwe la mji wa Charlestone wakati wa mafunzo ya Biblia.

Watu hao wote waliouawa walikuwa Wamarekani weusi. Mtuhumiwa wa mauaji,Roof ambaye ni Mmarekani mweupe amewekwa mahabusi kusubiri kufunguliwa mashitaka ya mauaji ya kudhamiria. Roof alietokea kwenye video, mahakamani, akionekana kuwa na majonzi. Mtu mmoja, Anthony Thompson miongoni mwa waliowapoteza ndugu zao,alimwambia Dylann Storm Roof "tunakusamehe" Ndungu yake Myra Thompson alikuwa miongoni mwa watu tisa waliopigwa risasi na kufa kwenye Kanisa kongwe la watu weusi katika mji wa Charlestone,South Carolina.

USA Schießerei in einer Kirche in South Carolina Reaktionen
Waumini wakishiriki maombi katika kanisa la African Methodist Emmanuel kulikotokea mauajiPicha: Reuters/G. Beahm

Thomson alimwambia,mtuhumiwa aitumie fursa waliyompa kutubu. Alimwambia mtuhumiwa atubu ili apate utulivu wa roho. Miongoni mwa waliouliwa ni Mchungaji Clementa Pinckney ambae pia alikuwa Seneta wa jimbo. Wengine walikuwa walimu, makocha, mkutubu, madiwani na waimbaji wa kwaya ya Kanisa kongwe la watu weusi, la Emanuel katika jimbo la South Carolina.

Katika hati ya ushahidi, iliyowasilishwa hapo jana polisi imesema Dylann Roof aliwapiga riasi watu hao wote tisa na pia imesema Roof alitoa kauli za uchochezi wa kibaguzi.

Mtuhumiwa aombewa:

Dada mmoja Alana Simmons ambae babu yake alikuwa miongoni mwa waliouawa amesema familia zao hazina nia ya kulipiza kisasi. Simmons amesema ingawa babu yake na wengine wamekufa kutokana na chuki,maombi yanayotolewa kwa ajili ya roho ya mtuhumiwa, ni ushahidi kwamba waliouliwa waliishi kwa upendo, na urithi wao utadumu daima. Simmons ameishukuru mahakama kwa kuhakikisha kwamba chuki haishindi.

Wakili wa Dylann Roof alitoa tamko la rambirambi kwa ndugu za watu waliouawa lakini pia alielezea mshtuko na mshangao juu ya kile kilichotukia. Wakili huyo alieleza jinsi alivyoguswa na yaliyosemwa na wale waliowapoteza watu wao. Mamia ya watu walijipanga mbele ya kanisa kuomboleza vifo vya watu hao tisa. Baadhi waliweka mashada ya maua na wengine walitoa matamko ya mshikamano.

Wakati huo huo wizara ya sheria ya Marekani imetangza kuwa itaanza uchunguzi ili kubainisha iwapo kadhia iliyotukia ilitokana na sababu za chuki au ugaidi wa kutokea ndani. Mtuhumiwa wa mauaji Roof alisema hivi karibuni kwamba watu weusi wanaichukua dunia na kwamba pana haja ya mtu kuchukua hatua kwa niaba ya watu weupe.

Mwandishi:Mtullya Abdu./ape

Mhariri: Bruce Amani