1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji alitamani kuuwa watu wengi

24 Julai 2016

Kijana Mjerumani - Muiran aliyewapiga risasi na kuwauwa watu tisa mjini Munich alikuwa mshambuliaji pekee ambaye alitamani mno kuuwa watu wengi na hajapata hamasa za itikadi kali za wanamgambo wa Kiislamu.

https://p.dw.com/p/1JUxc
Deutschland Tödliche Schießerei in München
Mkaazi wa mjini Munich akiweka maua katika eneo la tukio la mauajiPicha: Reuters/A. Wiegmann

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 18 , ambaye alizaliwa na kukulia nchini Ujerumani, aliwafyatulia risasi watu karibu na eneo linalotembelewa na watu wengi lenye maduka jioni ya Ijumaa, na kuzusha hali ya kufungwa maeneo katika mji mkuu wa jimbo la Bavaria.

Nach Schießerei in München
Maua na ujumbe uliowekwa na waombolezaji mjini MunichPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Joensson

Saba kati ya wahanga waliouwawa walikuwa vijana , ambao polisi imesema huenda aliwavuta wahanga wake kupitia ukurasa wa facebook uliodukuliwa katika kile ambacho ni kumbukumbu ya miaka mitano ya mashambulizi pacha yaliyofanywa na muuaji raia wa Norway Anders Breivik aliyewauwa watu 77.

Mashambulizi ya Munich , ambapo watu wengine 27 walijeruhiwa , baadhi wakiwa katika hali mbaya , ni tukio la tatu la matumizi ya nguvu dhidi ya raia katika Ulaya magharibi na la pili katika eneo la kusini mwa Ujerumani, katika muda wa siku nane.

Nach Schießerei in München Polizei
Polisi wakilinda doria katika eneo la maduka mjini MunichPicha: Reuters/A. Wiegmann

Rais wa ofisi inayoshughulikia uhalifu katika jimbo la Bavaria Robert Heimberger alisema mtu huyo mwenye silaha, ambaye vyombo vya habari nchini Ujerumani vimemtaja kwa jina la Ali David Sonboly , alikuwa na risasi zaidi ya 300 katika mfuko wake wa kubeba mgongoni na bastola wakati alipojiua.

Kufuatia upekuzi wa polisi katika chumba alikokuwa akiishi kijana huyo , ambako kitabu kulichotanabahisha azma ya mashambulizi ya kijana huyo kiligunduliwa , mkuu wa polisi wa Munich Hubertus Andrae aliondoa kabisa mahusiano wake na wanamgambo wa Kiislamu katika mashambulizi hayo.

Nach Schießerei in München
Wakaazi wa mjini Munich wakiweka maua katika eneo la tukioPicha: GGetty Images/AFP/C. Stache

Wakati huo huo maafisa waandamizi nchini Ujerumani wametoa wito leo(24.07.2016) kuchukuliwa hatua zaidi za udhibiti wa silaha baada ya shambulio la risasi siku ya Ijumaa mjini Munich.

"Tunapaswa kuendelea kufanya kila lililoko katika uwezo wetu na kudhibiti kikamilifu uwezekano wa kupatikana silaha," naibu kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel , kiongozi wa chama cha siasa za wastani cha Social Democratic , aliliambia shirika la vyombo vya habari la Funke Mediengruppe, ambalo linamiliki magazeti kadhaa nchini Ujerumani.

Nach Amoklauf am Olympia Einkaufszentrum in München Trauer
Watu wamekusanyika wakisoma maombolezi katika eneo lililowekwa maua mjini MunichPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Meyer

Gabriel alisema maafisa nchini Ujerumani wanachunguza, vipi kijana huyo mzaliwa wa Ujerumani mwenye uraia pacha wa Ujerumani na Iran alipata silaha licha ya ishara kwamba alikuwa na matatizo dhahiri ya akili.

"Suala la udhibiti wa silaha ni muhimu sana," Gabriel aliliambia shirika hilo linalomiliki magazeti mengi nchini Ujerumani.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /rtre

Mhariri: Sudi Mnette