Mshauri wa Trump kuhusu Usalama ajiuzulu
14 Februari 2017Mshauri huyo, Michael Flynn hapo awali alikuwa amekanusha kuhusisha suala la vikwazo dhidi ya Urusi, katika mazungumzo na balozi wa Urusi nchini Marekani Sergei Kislyak, wakati ambapo alikuwa hajaanza rasmi majukumu yake.
Hili linachukuliwa kama pigo kubwa kwa utawala wa Donald Trump ambao haujadumu hata kwa kipindi cha mwezi mmoja. Kwa siku kadhaa uvumi umekuwa ukienea, kwamba Flynn ambaye ni Jenerali mstaafu, alimdanganya Makamu Rais Mike Pence, ambaye alijitokeza hadharani kumtetea.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Flynn amesema ''bila kukusudia'' alimpa Makamu Rais ''taarifa ambazo sio kamilifu'' kuhusu mazungumzo yake ya simu na balozi Kislyak wa Urusi.
Ikulu ya White House mjini Washington imesema imemteuwa Luteni Jenerali Joseph Kellogg ambaye amekuwa mwenyekiti wa baraza la majenerali, kukaimu katika nafasi iliyoachwa wazi na Michael Flynn. Vyombo vya habari nchini Marekani viliripoti jana Jumatatu, kwamba utawala wa Donald Trump ulikwishatahadharishwa mapema mwaka huu kuhusu mahusiano kati ya Michael Flynn na Urusi.
Mwanzo wa maswali magumu
Maswali sasa yanaanza kuulizwa kuhusu watu katika utawala wa Marekani ambao walijua kuwepo kwa mazungumzo hayo, na kwa nini Rais Trump hakuchukua hatu mapema kumvua Flynn majukumu yake.
Kabla ya Michael Flynn kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu, msemaji wa Ikulu ya White House Sean Spencer alisisitiza kuwa Rais Trump hakufahamishwa chochote kuhusU mazungumzo kati ya Michael Flynn na balozi wa Urusi kuhusu vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo.
Yeyote atakayechukua nafasi ya Flynn ataliongoza Baraza la Usalama wa Taifa mnamo wakati utawala mchanga wa Rais Trump ukikabiliana na changamoto kubwa, likiwemo jaribio la hivi karibuni la makombora ya kivita lililofanywa na Korea Kaskazini.
Vile vile utawala wa Trump unaogelea katika dimbwi la msukosuko uliotokana na amri ya rais huyo kuwapiga marufuku kuingia Marekani, watu wote kutoka mataifa saba yenye waislamu wengi, amri ambayo hivi sasa imesimamishwa na mahakama.
Michael Flynn ambaye alikuwa muungaji mkubwa wa Donald Trump tangu hatua za awali za kampeni yake, amekuwa akihimiza msimamo mkali dhidi ya Iran na kulegeza sera dhidi ya Urusi, mtazamo ambao ni kunyume kabisa na ule wa utawala uliotangulia wa Rais Barack Obama.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, afpe
Mhariri: Zainab Aziz