1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshindi huenda asitawale.

Mohamed Dahman20 Julai 2007

Chama tawala nchini Uturuki chenye mizizi ya Kiislam hivi karibuni kitaweka rekodi yake kwenye mtihani wakati wa uchaguzi wa bunge uliohodhiwa na dhima ya dini katika maisha ya wananchi na uwezekano wa kuingilia kijeshi kwenye kinamasi cha Iraq.

https://p.dw.com/p/CHAn
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri wa mambo ya nje Abdulla Gul wa chama tawala cha AKP.
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri wa mambo ya nje Abdulla Gul wa chama tawala cha AKP.Picha: AP

Huenda chama hicho kikashinda lakini sio kutawala!

Wakati wapiga kura milioni 44 wakipiga kura hapo Jumapili ya tarehe 22 mwezi wa Julai matarajio ni kwamba chama tawala cha Sheria na Maendeleo AKP cha Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan kinaweza kushinda tena lakini kwa upungufu wa wingi wa viti kwenye bunge la viti 550.

Uchunguzi wa maoni katika gazeti la kila siku la Hurriyat unakipa chama hicho cha AKP kama asilimia 30 ya kura ikiwa chini kutoka asilimia 34 na viti vyake kupunguwa kuwa 300 na ushee kidogo kutoka viti vyake vya hivi sasa 353.

Chama kikuu cha upinzani cha Republican cha Wananchi CHP ambacho sio cha kidini kinatazamiwa kuongeza asilimia yake 20 ya kura na chama cha sera kali za mrengo wa kulia cha MHP kinatarajiwa kuvuka kikwazo cha kujipatia asilimia 10 ya kura kuingia bungeni.

Uchaguzi huu ambao unafanyika miezi mitatu mapema kabla ya wakati wake kutokana na kikwazo cha bunge juu ya uchaguzi wa rais mpya unakuja kufuatia kampeni kali na kingamizi kati ya makundi yasio ya kidini dhidi ya agenda ya chama cha AKP.Uchaguzi huu utakuwa unafanyika chini ya uangalizi makinifu wa jeshi lenye nguvu kubwa lisilokuwa na misimamo ya kidini.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni kioja hata kama chama hicho tawala cha AKP kitajipatia ushindi wa kutosha kutawala yumkini kisiunde serikali na huenda ukafanyika uchaguzi mwengine katika kipindi cha wiki chache.

Hii ni kwa sababu kazi kuu ya bunge jipya baada ya kufunguliwa itakuwa ni kumchaguwa rais ambaye naye atamteuwa waziri mkuu.Lakini chama cha AKP kitahitaji viti 367 ili mgombea wake aweze kuteuliwa au itabidi wafikie muafaka wa mgombea. Kwa hivi sasa mambo hayo yote mawili inaonekana hayawezi kutokea jambo ambalo yumkini likapelekea kufanyika kwa uchaguzi mpya wa bunge katika kipindi kisichozidi miezi miwili.

Baadhi ya watu wanaona kuna hatari iwapo chama cha AKP kitatowa rais.Gulsun Zeytinoglo mjumbe wa zamani wa Bodi ya Wajasiriamali wa Kike anasema Jamhuri ya Uturuki itakuwa kwenye vurugu.

Mwandishi wa Kifaransa alieko Istanbul Jerome Bastion ambaye ni mchambuzi wa siasa za Uturuki anasema jeshi halitomkubali rais wa chama cha AKP na kwamba mapinduzi ya moja kwa moja sio jambo linaloyuminika kutokea lakini jeshi bado lina njia nyengine kumpinga rais mwenye mawazo ya siasa kali za Kiislam.

Magenerali walifanya hivyo hapo tarehe 27 mwezi wa April masaa mchache baada ya waziri wa mambo ya nje Abdullah Gul ambaye Muislamu wa siasa kali wa zamani chupuchupu awe rais kwa kasoro ya kura 20.Katika tangazo la usiku wa manane kwenye tovuti yake ambalo tokea wakati huo limepewa jina la mapinduzi kwenye mtandao jeshi lilisema wazi kwamba Gul ambaye mke wake hujifunikia hijabu kichwani hakubaliki.

Uhusiano wake na chama tawala cha AKP umekuwa wa mvutano kutokana na kusambaa kwa ushawishi wa Kiislam katika maisha ya watu.Chama hicho tawala kilikuwa kikishinikiza jeshi kuwa na dhima ndogo katika masuala ya kuongoza nchi kwa kutaja kanuni za demokrasia za Umoja wa Ulaya ambazo Uturuki inalazimika kufuata ili kuwa nchi ya kwanza ya Kiislam mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Eneo jengine la mvutano kati yao ni suala la ugaidi ambao umekuwa ukiongezeka kutoka chama cha waasi wa Kikurdi walioko Iraq cha PKK wanaojipenyeza Uturuki ambapo jeshi limependekeza kujiingiza kaskazini mwa Iraq wakati serikali ikizingatia mashaka ya Marekani na Umoja wa Ulaya imekataa kutowa kibali.

Erdogan amesema Uturuki kwanza lazima ipambane na ugaidi wa Kikurdi uliomo ndani ya nchi kabla ya kujitumbukiza kwenye jambo wasilolijuwa nchini Iraq.