1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshindi wa urais Sri Lanka kuapishwa

9 Januari 2015

Mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Sri Lanka, Maithripala Sirisena, anaapishwa leo (09.01.2015), baada ya rais aliyeko madarakani Mahinda Rajapaksa kukubali kushindwa katika uchaguzi huo uliofanyika jana.

https://p.dw.com/p/1EHlE
Mshindi wa urais Sri Lanka, Maithripala Sirisena
Mshindi wa urais Sri Lanka, Maithripala SirisenaPicha: picture-alliance/AP/Eranga Jayawardena

Maithripala Sirisena, waziri wa zamani wa afya wa Sri Lanka, anatarajiwa kuapishwa baadae leo jioni katika uwanja wa Uhuru. Msaidizi wa ngazi ya juu wa Rajapaksa, amesema kiongozi huyo anayeondoka madarakani, amekubali kushindwa baada ya uamuzi huo wa wapiga kura. Matokeo hayo ni pigo kubwa kwa kiongozi huyo aliyekuwa na uhakika kuwa atashinda, baada ya kuitisha uchaguzi wa mapema mwezi Novemba.

Katibu wa habari wa Rais, Vijayananda Herath ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa Rajapaksa amekubali kushindwa na amehakikisha kuwa kutakuwa na kipindi salama cha mpito wakati anapokabidhi madaraka. Amesema Rajapaksa tayari ameanza kuondoka katika makaazi yake rasmi ikiwa ni ishara ya kuonyesha kuwa amekubali kushindwa.

Akizungumza katika ofisi za tume ya uchaguzi mjini Colombo, Sirisena amempongeza na kumshukuru Rajapaksa kwa kukubali kushindwa. Amesema hali hiyo inaonyesha kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. Kamishna wa uchaguzi wa Sri Lanka, Mahinda Deshapriya, alimtangaza Sirisena kuwa mshindi baada ya kupata asilimia 51.28 ya kura zilizopigwa dhidi ya Rajapaksa, aliyepata asilimia 47.58.

Raisanayeondoka madarakani Mahinda Rajapaksa
Rais anayeondoka madarakani Mahinda RajapaksaPicha: picture alliance/Photoshot

Ranil Wickremesingle ambaye huenda akateuliwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, amesema dalili zinaonyesha kutakuwa na makabidhiano mazuri ya madaraka. Ranil ambaye ni kiongozi wa upande wa upinzani katika bunge la Sri Lanka, amesema watu wanataka mfumo mpya wa siasa. ''Watu wametupa ujumbe wa mabadiliko na lazima tuuzingatie ujumbe huo. Lazima tufanye hivyo, amesema Ranil.''

Sirisena azungumza na Rajapaksa kwa simu

Ranil mbunge wa chama cha upinzani cha United National-UNP, amesema Sirisena alizungumza kwa njia ya simu na Rajapaksa baada ya matokeo kutangazwa. Aidha, mbunge wa chama cha Rajapaksa cha Freedom, Thilanga Sumathipala, amesema kiongozi huyo aliitisha mkutano na baraza lake la mawaziri na alionekana mtu mwenye hisia sana. Kwa mujibu wa mbunge huyo, hatua hiyo iliwafanya mawaziri wengi wabubujikwe na machozi.

Hata hivyo, Sirisena amewataka wafuasi wake kusherehekea ushindi wake kwa amani bila ya kusababisha madhara kwa wengine. Ameahidi kufanya mageuzi katika kipingele cha mamlaka ya rais, kwa kuhamishia vipengele hivyo katika bunge.

Wananchi wa Sri Lanka wakipiga kura, Januari 8, 2015.
Wananchi wa Sri Lanka wakipiga kura, Januari 8, 2015.Picha: Reuters/Dinuka Liyanawatte

Wakati wa kampeni, Sirisena alimuonya Rajapaksa kuhusu kubadilisha njia zake za uongozi, la sivyo atakuwa katika hatari kubwa ya machafuko. Anasema alikuwa akiiongoza nchi kuelekea kwenye njia ya uharibifu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amepongeza hatua ya kukabidhiana madaraka mapema na kwamba yuko tayari kufanya kazi na serikali mpya. Uchaguzi wa Sri Lanka ulipata shinikizo la kimataifa, huku Marekani ikimtaka Rajapaksa kuhakikisha unafanyika kwa amani.

Uchaguzi wa Sri Lanka umefanyika siku chache kabla kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis hajazuru katika kisiwa hicho.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga