1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa wa mashambulizi ya Berlin auawa Milan

Mohammed Khelef
23 Desemba 2016

Taarifa zinasema kuwa mtuhumiwa mkuu wa mashambulizi ya Berlin, Anis Amri, ameuawa kwenye makabiliano ya risasi kati yake na polisi wa Italia, mjini Milan.

https://p.dw.com/p/2Un5U
Italien Mutmaßlicher Berliner Attentäter in Mailand getötet
Picha: picture-alliance/dpa/Daniele Bennati/B&V

Taarifa za vyombo vya habari nchini Italia zinasema mshukiwa huyo, raia wa Tunisia, Anis Amri, ameuawa alfajiri ya leo katika kitongoji cha Sesto san Giovani mjini Milan.

Kulingana na taarifa hizo, Amri alisimamishwa katika msako wa kawaida wa polisi, lakini badala ya kuonesha vitambulisho vyake, alichomoa bunduki, hatua iliyozusha mapambano ya risasi baina yake na polisi.

Vyanzo tofauti vimelithibitishia shirika la habari la ANSA kuuawa kwa mshukiwa huyo.

Polisi mmoja amearifiwa kujeruhiwa katika mapambano hayo. 

Mtunisia huyo mwenye miaka 24 alikuwa akisakwa tangu alipouwa watu 12 na kujeruhi wengine zaidi ya 30 katika soko la Krismasi, katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, mapema wiki hii.

Hayo yanajiri huku ndugu wawili wazaliwa wa Kosovo wakitiwa nguvuni kwa tuhuma za kupanga mashambulizi kwenye jengo moja la maduka mengi magharibi mwa Ujerumani, siku chache baada ya mashambulizi yaliyouwa watu 12 kwenye soko la Krismasi katika mji mkuu, Berlin.

Polisi inasema wanaume hao wenye umri wa miaka 28 na 31, walitiwa nguvuni mjini Duisburg, usiku wa kuamkia leo.

Mamlaka zinashuku kuwa washukiwa hao walikuwa wanapanga kulishambulia jengo la maduka la Centro karibu na mji wa Oberhausen. Kwa sasa, polisi inachunguza dhamira ya ndugu hao na endapo walikuwa wana wasaidizi wao.

Kukamatwa kwa watu hao kulitokana na taarifa za kiintelijensia, kwa mujibu wa polisi. Kampuni ya Centro ni maarufu sana nchini Ujerumani, ikiwa na maduka yapatayo 250.