1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa wa mauaji ya Ufaransa 'kujisalimisha'

21 Machi 2012

Polisi watatu wamejeruhiwa katika utupianaji risasi kati yao na mtu anayeshukiwa kuhusika na mauaji ya watu wanne katika skuli ya Kiyahudi hapo Jumatatu na wanajeshi watatu kusini magharibi mwa nchi hiyo wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/14OOA
Polisi wakiuzingira mtaa ambako mtu anayeshukiwa kwa mauaji anaishi.
Polisi wakiuzingira mtaa ambako mtu anayeshukiwa kwa mauaji anaishi.Picha: REUTERS

Polisi wenye silaha nzito, wakiwa wamevalia nguo za kujikinga na risasi, wameivamia nyumba moja katika kiunga kilicho kilomita chache kutoka skuli ya Kiyahudi ya Ozar Hatorah, ambako mauaji ya Jumatatu yalitokea.

Mashahidi wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba walisikia milio kadhaa ya risasi mwendo wa saa 10 na dakika 40 alfajiri kwa saa za Ulaya ya Kati, sawa na saa 12 na dakika 40 asubuhi Afrika Mashariki.

Polisi waliojeruhiwa wanasemekana kupigwa risasi za shingo na bega, lakini haijuilikani wameumia kwa kiasi gani. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Claude Gueant, amesema Mohammed Merah mwenye miaka 24 na aliye na asili ya Algeria, ana mafungamano na al-Qaida, akiwa ameshazitembelea Pakistan na Afghanistan mara kadhaa, na kwamba alisema analipiza kisasi kwa ushiriki wa jeshi la Ufaransa nje ya nchi.

Merah alitaka kulipiza kisasi

Akiwa eneo la tukio, Guaent amewaambia waandishi wa habari na hapa namnukuu: "Kijana huyo anadai kuwa yeye ni mpiganaji wa Jihad na ni al-Qaida. Alitaka kulipiza kisasi kwa ajili ya watoto wa Kipalestina na pia dhidi ya jeshi la Ufaransa kwa kuingilia wake kwenye mataifa ya kigeni." Mwisho wa kumnukuu.

Majirani katika eneo la tukio wakizungumza na waandishi wa habari.
Majirani katika eneo la tukio wakizungumza na waandishi wa habari.Picha: REUTERS

Gueant amesema polisi pia wamemshikilia kaka wa mshambuliaji huyo, ambaye ni raia wa Ufaransa kutoka mji wa Toulouse, baada ya kugundua anwani ya barua-pepe iliyomuunganisha na mwanajeshi wa kwanza kuuawa.

Mama wa mshambuliaji alipelekwa pia katika eneo la tukio, kiunga cha kaskazini cha Toulouse, kusaidia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kati ya polisi na mshambuliaji huyo, wakati taarifa hii inakwenda mitamboni. Matarajio ni kwamba mshambuliaji huyo atajisalimisha kwa polisi kufikia jioni ya leo. Mapema alikuwa amekubali kuitupa nje bastola yake kwa mabadilishano na kifaa cha mawasiliano, lakini bado alikuwa na bunduki aina ya AK47.

Rais Nicolas Sarkozy alijulishwa juu ya hali ilivyo wakati uvamizi ulipoanza. Wachunguzi wanaamini kuwa mshambuliaji wa Jumatatu ndiye yule yule aliyewapiga risasi na kuwauwa wanajeshi watatu wa Kifaransa wenye asili ya Kaskazini mwa Afrika wiki iliyopita huko huko Toulouse na mji wa karibu wa Montauban.

Bunduki aina ya Colt 45 ilitumika katika matukio yote matatu na ambapo muhusika alikuwa akiendesha pikipiki aina ya Yamaha akiwa ameficha uso wake na kofia la chuma.

Mauaji haya yametokea wiki tano tu kabla ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais, ambapo masuala ya wahamiaji na Uislamu yamekuwa muhimu sana, huku Sarkozy akipigania kushinda kura za mpinzani wake mwenye msimamo mkali dhidi ya mambo hayo, Marine Le Pen.

Wakati hayo yakitokea, miili ya watoto watatu na mwalimu mmoja inatarajiwa kuzikwa leo nchini Israel, baada ya kusafirishwa kwa ndege kutoka Ufaransa hapo jana. Wanajeshi watatu waliouawa nao pia watazikwa kwa heshima kamili za kijeshi hivi leo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba