1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msimamo juu ya Libya kitisho kwa uhusiano wa Ulaya, Afrika

16 Septemba 2011

Licha ya kuwa kwake umuhimu wa kimkakati katika uhusiano wa Ulaya na Afrika, tafauti ya kimsimamo kati ya Afrika ya Kusini na Ulaya kuelekea mgogoro wa Libya yaonekana kuwa kizuizi katika uimarishaji wa mahusiano hayo.

https://p.dw.com/p/12aDW
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya KusiniPicha: dapd

Afrika ya Kusini, ambayo ni mwenyeji wa mkutano huu baina ya taifa hilo na Umoja wa Ulaya, inapigania sana kuyaimarisha mahusiano haya. Lakini hili halimzuii Rais Jacob Zuma kurejelea msimamo wake dhidi ya siasa za Umoja wa Ulaya kuelekea Libya.

Tangu mwanzoni mwa mgogoro wa Libya, Rais Zuma amebakia na msimamo kwamba mataifa ya Magharibi yalilitumia vibaya Azimio Namba 1973 la Umoja wa Mataifa juu ya Libya.

Mtangulizi wa Rais Zuma, Thabo Mbeki anadai kwamba kusema kuwa uingiliaji kati wa NATO nchini Libya ulikuwa muhimu kwa kuwa Muammar Gaddafi alitaka kuigeuza Libya bwawa la damu ya raia, ulikuwa uongo. Lakini angalau katika mwanzo wa mkutano huu, Rais Zuma hakutaka kwenda undani wa suala la Libya, pale alipozungumza na waandishi wa habari.

"Kwa ujumla sote tumefurahishwa sana na kile kilichomo kwenye ajenda na undani wa mijadala yenyewe." Alisema Rais Zuma.

Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini (kushoto) na mwenyekiti wa Kamishna wa Umoja wa Afrika Ramtane Lamamra.
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini (kushoto) na mwenyekiti wa Kamishna wa Umoja wa Afrika Ramtane Lamamra.Picha: dapd

Masuala ya Cote d'Ivoire, Zimbabwe na Libya ni mambo yenye mvutano mkubwa wa kimaoni kati ya pande hizi mbili. Afrika ya Kusini na Umoja wa Afrika hadi sasa hawajalitambua Baraza la Mpito la Libya.

Umoja wa Ulaya, kwa upande wake, imeshalitambua Baraza hilo kitambo mno kama wawakilishi halali wa watu wa Libya, pamoja na matokeo yote, ikiwemo uwakilishi kwenye Umoja wa Mataifa.

"Katika aina ya uhusiano wa kimkakati tulionao, tunapaswa kuwa wazi katika masuala hayo na nafikiri tumekubaliana katika baadhi ya mambo muhimu. Sasa kunahitajika kuwepo kwa maridhiano ya kitaifa na hatua za maendeleo nchini Libya. Kwa hivyo, nafikiri, tunaweza kukubaliana juu ya ushiriki wetu katika ujenzi wa mustakabali wa Libya." Alisema Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barosso.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy anaamini kuwa ujenzi wa Libya mpya ni suala la Walibya wenyewe na kwamba tafauti iliyopo baina ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika ni za kawaida na haziwezi kuzuia ujenzi huo, kwani hata kama pande hizi mbili zilitafautiana hapo mwanzoni, bado zina mawazi mamoja kwenye mustakabali wa Libya.

Mchakato wa kidemokrasia, uchaguzi, na serikali yenye uwakilishi wa watu wote na inayowajibika ni mambo yanayotakiwa na pande zote mbili. Ingawa kwa upande wa Afrika ya Kusini, suala ni ikiwa kwa kiasi gani Umoja wa Ulaya utawashinikiza waasi kutekeleza haya.

"Si lazima tuwasukume kufanya jambo hilo. Wenyewe Baraza la Mpito wameandika katika barua yao kwa Umoja wa Afrika, kwamba wako tayari ndani ya kipindi kifupi kijacho kuunda serikali yenye uwakilishi wa Walibya wote." Amesema Rompuy.

Jambo hili ikiwa litafanyika, linaweza kuwaridhisha na kuleta mwanga mpya katika mahusiano kati ya Umoja wa Afrika na Baraza la Mpito nchini Libya.

Mwandishi: Claus Stäcker/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo