1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu kondomu tofauti na hali halisi

19 Machi 2009

Miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari magazetini Ujerumani leo siku ya Alkhamisi ni matamshi ya Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 kuhusu matumizi ya kondomu.

https://p.dw.com/p/HFOP

Mada nyingine ni uamuzi uliopitishwa na Mahakama Kuu ya Ujerumani kuhusu malipo ya akina mama wenye watoto baada ya ndoa kuvunjika.Lakini tutaanza na matamshi ya Papa Benedikt yaliyozusha midahalo mikali sehemu mbali mbali duniani. Gazeti la AUGSBURGER ALLGEMEINE linasema:

"Ulimwengu unashangazwa na msimamo wa desturi wa kanisa kuhusu matumizi ya kondomu.Na barani Afrika ambako watu wengi wameambukizwa UKIMWI, msimamo wa Kanisa la Katoliki kuhusu matumizi ya kondomu una athari zake. Mgogoro huo unaolitenga kanisa hilo na hali halisi ya mambo hauwezi kuondoshwa kwa matamshi fulani tu katika mahojiano.Lakini suala la kondomu si mada pekee kulitenganisha Kanisa la Katoliki na ulimwengu wa hivi sasa. Na ionekanavyo linataka kuendelea na hali hiyo."

Gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG likiandika kuhusu mada hiyo hiyo linaeleza hivi:

"Kwanza ulikuwa mgogoro wa Williamson aliekanusha kutokea kwa mauaji ya kuwaangamiza Wayahudi-Holocaust na sasa kondomu na UKIMWI. Yadhihirika kuwa Papa Benedikt hajitengi na waumini wake tu bali hata na ukweli halisi wa mambo. Msimamo wa Vatikan kuhimiza uaminifu katika ndoa na kuzuia uhusiano nje ya ndoa unaeleweka. Vile vile, inafahamika kuwa matumizi ya kondomu pekee,sio suluhisho kwa tatizo la UKIMWI. Lakini,kutamka kuwa matumizi ya kondomu huifanya hali hiyo kuwa mbaya zaidi ni upuuzi."

Sasa tunabadili mada na tunatupia jicho gazeti la BILD ZEITUNG linalosema kwamba zamani ilijulikana wazi wazi kuwa ndoa inapovunjika mwanamke hushughulikia ulezi wa watoto na mwanamume hulipia gharama za mtoto na mama. Lakini hiyo jana,Mahakama Kuu ya Ujerumani ilipitisha uamuzi uliowahamakisha akina mama wengi. Gazeti la BILD ZEITUNG likieleza maoni yake limeandika:

"Wanawake wasitegemee tena kulipwa pesa za matumizi na waume wao wa zamani ndoa inapovunjika. Wanapaswa kwenda kufanya kazi hata ikiwa wana watoto. Baba atawalipia watoto lakini sio mama. Wapinzani wa sheria mpya wamepaaza sauti kuwa ndoa haitiwi maanani tena. Lakini huo ni upuuzi. Ndoa itaendelea kulindwa kisheria lakini kuhifadhi hali ya maisha ya mwanamke hata baada ya ndoa kuvunjika ni jambo la kale. Kwa hivyo, ni bora kwa wanawake kuzingatia kwa makini kabla ya kuamua kubakia nyumbani kwa ulezi wa watoto baada ya kuolewa.Ndoa ni jambo zuri na ni sahihi, lakini sio tena chombo cha kujihakikishia pato la kuendesha maisha." Hayo ni maoni ya gazeti la BILD ZEITUNG.

Mwandishi: P.Martin/DPA

Mhariri: Othman Miraji