1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msumbiji na juhudi za kudhibiti maafa ya mafuriko

P.Martin4 Mei 2008

Idadi ya watu waliopoteza maisha yao kwa ugonjwa wa kipindupindu kufuatia mafuriko ya hivi karibuni nchini Msumbiji,ni kubwa zaidi kuliko wale walioteketea katika mafuriko hayo.

https://p.dw.com/p/DtDj
Blick über die mosambikanische Hauptstadt Maputo Foto: P. Reategui
Maputo,mji mkuu wa Msumbiji.Picha: P. Reategui

Mito mingi,hasa katika maeneo ya kati na kaskazini mwa nchi,ilifurika kwa sababu ya mvua kubwa za Desemba,Januari na Februari pamoja na kimbunga Jokwe kilichotokea mapema mwezi Machi.Inaaminiwa kuwa watu wapatao kama dazeni moja walipoteza maisha yao katika mafuriko na watatu waliliwa na mamba.Lakini ni watu 72 waliofariki kwa kipindupindu na idadi kama hiyo pia walipoteza maisha yao kwa sababu ya magonjwa yanayoambukizwa kupitia maji machafu, kama vile tumbo la kuhara damu.Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la madaktari wanaotoa misaada-MSF.

Hesabu hizo zaonyesha kuwa serikali ya Msumbiji sasa imefanikiwa kupunguza maafa yanayozuka pale pale mafuriko yanapotokea,lakini inahangaika kudhibiti magonjwa yanayoenea baada ya mafuriko.Ingawa mvua kubwa kama za safari hii hazijawahi kushuhudiwa tangu miaka na miaka,serikali ilifanikiwa kuwahamisha takriban watu wote kutoka maeneo yaliyokuwa katika hatari ya kufurika.Kinyume na ilivyokuwa wakati wa mafuriko ya mwaka 2000 na 2007,safari hii zaidi ya watu 100,000 walihamishwa na kupelekwa maeneo ya usalama yaliyokuwa mbali na mito.Wengine walihamishwa kwa nguvu.Mafuriko yalipoanza kupunguka,kimbunga Jokwe kilivuma katika mwambao wa Nampula mji ulio kaskazini mwa Msumbiji.Kimbunga hicho kiliua watu 17 na maelfu wengine walipoteza maskani zao.

Sasa serikali ndio inataka kujenga vijiji vya kudumu katika maeneo ambako watu walipelekwa kukimbia mafuriko. Kwani katika miezi ya hivi karibuni zaidi ya nyumba 20,000 zilisombwa na maji.Lengo ni kuzuia operesheni za uokozi za mara kwa mara kwani mafuriko kama hayo hutokea takriban kila mwaka nchini humo.Lakini wanavijiji hawataki kubakia katika maeneo hayo mapya kwani hiyo humaanisha watakuwa mbali na mashamba yao yaliyo kingoni na mito.Kwa hivyo serikali imezindua mpango wa kuwavutia wale waliobaki katika maeneo hayo mapya ambao ni kama 30,000.

Wakaazi hao wanahimizwa kuweka mabomba ya maji,kujenga nyumba na miundo mbinu inayohitajiwa kwa ajili ya usafi wa kimsingi.Familia zinazofanya kazi hizo hupatiwa chakula cha kutosha kuendesha maisha yao. Serikali haitosaidia tu kuanzisha miradi kamili ya usafi na kufungua zahanati,bali wakaazi hao watapatiwa pia zana za ujenzi zenye bei nafuu na wataonyeshwa njia ya kuzijenga nyumba hizo.

Serikali ilitambua kuwa mafuriko yatasababisha ugonjwa wa kipindupindu.Na kweli mafuriko yalipoanza kupunguka tu,kesi nyingi za kipindipindu ziliripotiwa hasa katika Wilaya ya Mutarara,iliyo kaskazini mwa Msumbiji karibu na mpaka wa Malawi.Lakini Msumbiji ni nchi masikini na haina uwezo wa kuwapatia wananchi wote,miundo mbinu ya kutosha katika sekta ya usafi.