1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtaka cha mvunguni lazima ainame

19 Mei 2011

Miongoni mwa mada zilizoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani leo, Alkhamisi, ni mpango wa mageuzi makubwa yanayopangwa kufanywa katika jeshi la Ujerumani, Bundeswehr.

https://p.dw.com/p/ROpY
Verteidigungsminister Thomas de Maiziere (CDU) steht am Mittwoch (18.05.11) in der Julius-Leber-Kaserne in Berlin bei einem Statement zur Bundeswehrreform hinter dem Rednerpult. De Maiziere hat die Organisation und die Strukturen der Bundeswehr fuer derzeitige und kuenftige Aufgaben als "unzureichend" bezeichnet. Das betreffe die Faehigkeiten, die Finanzierung und Fuehrungsstruktur, sagte der CDU-Politiker bei der Vorstellung seiner Eckpunkte zur Streitkraeftereform am Mittwoch in Berlin. (zu dapd-Text) Foto: Clemens Bilan/dapd
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Thomas de MaizièrePicha: dapd

Mada nyingine ni mzozo wa madeni wa baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya katika kanda inayotumia sarafu ya Euro. Tukianza na mageuzi ya Bundeswehr, gazeti la NEUE OSNABRÜCKER linasema:

"Hakuna waziri wa ulinzi wa Ujerumani aliepata kueleza kinagaubaga matatizo ya jeshi la Ujerumani, kama alivyofanya waziri wa sasa, Thomas de Maiziére. Kwa sehemu fulani, maamuzi yanashindwa kupitishwa kwa sababu ya kuwepo kwa viongozi wengi mno pamoja na urasimu mkubwa."

Gazeti la NEUE WESTFÄLISCHE vile vile linasema:

"Tatizo la jeshi ni kwamba mabosi ni wengi na wanajeshi ni wachache. Kuambatana na mageuzi yatakayofanywa katika jeshi la Ujerumani, idadi ya viongozi wa ngazi za juu itapunguzwa. Bila shaka, uamuzi huo utakumbana na upinzani mkali. Kazi inayomkabili waziri mpya wa ulinzi ni kubwa mno. Kubadili mfumo wa jeshi na, wakati huo huo, kupunguza gharama zake na kuwavutia vijana wanaojitolea kuwa wanajeshi."

Kwa maoni ya DER NEUE TAG, waziri wa ulinzi de Maiziére anakabiliwa na kazi ngumu.

"Waziri huyo atakumbana na wabunge, mawaziri wenzake na wawakilishi wa serikali za mitaa na majimbo atakapotaja idara na miji itakayoathirika katika mpango wa kupunguza wafanyakazi na kufungwa kwa baadhi ya vituo vya jeshi. Bila shaka, hata viwanda vya silaha havitobaki kimya."

"Sasa tunageukia mada nyingine iliyoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani hii leo. Mzozo wa fedha katika kanda ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro barani Ulaya. Gazeti la BILD ZEITUNG linakumbusha hivi :

"Wahenga wanasema, mtaka cha mvunguni lazima ainame. Kwa maneno mengine, nchi zenye madeni katika kanda ya Euro na zinazotaka msaada wa fedha kutoka Ujerumani, zinapaswa pia kujitahidi zaidi kupunguza gharama zao, kupandisha umri wa kustaafu na kupunguza siku za likizo. Hatua hizo zitasaidia kuimarisha uchumi wao."

Kansela wa Ujerumani hafanyi kosa, anapozitaka nchi zenye madeni kuchukua hatua kama hizo. BILD ZEITUNG linakumbuisha hivi:

"Miaka hii iliyopita Ujerumani imebana matumizi yake kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Wajerumani wamekubali kufanya kazi bila ya kuapta nyongeza ya mishahara, na sasa imependekezwa kuwa wafanye kazi mpaka umri wa miaka 69. Uchumi wa Ujerumani haukuimarika hivi hivi bali umepatikana kwa kazi ngumu na kwa kujitolea. Kwa hivyo haiwezekani kuwa mmoja anajihini na wengine wanafaidika."

Mwandishi:MartinPrema/dpa

Mhariri: Miraji Othman