1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtazamo wa Hollande kuhusu Ulaya watia mashaka

20 Aprili 2012

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani angelipendelea rafiki yake, Nicolas Sarkozy kushinda uchaguzi wa Ufaransa, lakini kura za maoni zinamuonesha François Hollande kuwa ndiye mwenye nafasi nzuri zaidi.

https://p.dw.com/p/14iA4
Mgombea wa urais wa Ufaransa, Francois Hollande.
Mgombea wa urais wa Ufaransa, Francois Hollande.Picha: picture-alliance/dpa

Kimsingi siasa za nje na za Ulaya zina nafasi ndogo sana kwenye kampeni za uchaguzi huu, lakini zinapohusishwa na siasa za ndani za Ufaransa, pana tafauti kubwa kati ya msoshalisti Hollande na mhafidhina Sarkozy.

Matarajio ya wachambuzi wengi ni kwamba uchaguzi huu ndio nafasi ya mwisho ya kuifanya demokrasia ya Ufaransa iwe ya kisasa zaidi, na zaidi kurekebisha sheria za fedha kufikia majira ya kiangazi yanayokuja hivi punde.

Miongoni mwa masuala yanayoulizwa na wengi ni ikiwa Ufaransa itakuwa muhanga mwengine wa masoko ya fedha. Kwa Hollande, suala hili linalozuka siku chache kabla ya uchaguzi, limekuja wakati sio.

"Ufaransa haina tatizo kabisa na uuzaji wa dhamana zake. Japokuwa tatizo ni kuwa tunalipa riba kubwa zaidi, lakini tuko mbali kabisa na ile hali inayoyakumba mataifa mengine ya Ulaya." Anasema mshauri wa chama cha Kisoshalisti, Jacques-Pierre Gougeon:

Na ama kuhusu suala la ikiwa Ufaransa iongoze kujitolea mstari wa mbele katika Umoja wa Ulaya, jambo hilo ni ndoto kwa mgombea wa Kisoshalisti, François Hollande, ambaye anapendelea aina ya mahusiano legelege sana na majirani zake.

"Wahafidhina wameitawala Ulaya kwa muda mrefu sana. Uwiano wenu ni mbaya sana. Ulaya inapitia katika mgogoro mbaya sana wa kifedha katika historia yake. Nami nimeshathibitishiwa na wachambuzi wengi na hapa nitasema tena. Nitapigania kupatikana kwa mkataba mpya wa masuala ya fedha barani Ulaya." Anasema Hollande.

Tangazo la matumaini

Tangazo hili linatoa matumaini kwa serikali ya Angela Merkel wa Ujerumani, ambaye amekuwa akipigania kuwepo kwa udhibiti mkali sana wa nidhamu ya bajeti inayosimamiwa na Umoja wa Ulaya, na sio na nchi binafsi. Lakini halipendelewi hata kidogo na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya.

Mtetezi wa kiti cha urais, Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.
Mtetezi wa kiti cha urais, Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.Picha: Reuters

Lakini suala la kutafuta makubaliano mapya ya Umoja wa Ulaya, haliwavutii wafuasi wengi wa mrengo wa kushoto, ambao kura zao zinategemewa kuleta ushindi ama kwa Sarkozy au kwa Hollande katika duru ya pili ya uchaguzi.

Sababu wote wawili, wanategemea kura za wagombea wengine ambao hawataingia kwenye duru ya pili kushinda. Sarkozy anategemea kura za wafuasi wa mgombea mwenye msimamo mkali wa kulia, Marine Le Pen, wakati Hollande anategemea kura za Jean-Luc Mélenchon.

Haifahamiki hadi sasa, endapo Hollande akichaguliwa kuwa rais atafanikiwa mangapi katika yale anayoyaahidi linapohusika suala la Umoja wa Ulaya, lakini ni wazi kwamba mabadiliko yoyote yatakayofanywa kwenye Mkataba wa mwaka 1997 wa Amsterdam, yatakuwa na faida kwake binafsi.

Jambo hilo, wanasema wachambuzi, linaweza kuwa alama kubwa ya mafanikio ya Hollande, ambaye maingiliano makubwa sana na majirani wa Ufaransa katika Umoja wa Ulaya au hata kwenye sera za nje.

Lakini uhusiano wa mhafidhina Merkel na msoshalisti Hollande unasubiriwa kwa hamu kuonekana utazaa matunda gani katika Umoja wa Ulaya, ikizingatiwa kwamba Kansela Merkel ameonekana wazi kumuunga mkono Sarkozy, ambaye hana nafasi kubwa ya kushinda tena.

Mwandishi: Andreas Noll
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdulrahman