1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtoto wa Charles Taylor apatwa na hatia ya kuwatesa watu

Kalyango Siraj31 Oktoba 2008

Hukumu yake ni kifungo cha maisha

https://p.dw.com/p/Fl4t
Charles Taylor rais wa zamani wa Liberia.Mtoto wake Taylor Jr apatwa na hatia ya kuwatesa watu chini ya utawala wake kati ya mwaka 1997 na 2003Picha: AP

Mtoto wa Charles Taylor, rais wa amani wa Liberia, amepatikana na hatia ya kuwatesa watu wakati wa utawala wa babake.Hukumu hiyo imefanyika nchini Marekani na hii ndio mara ya kwanza kwa mahakama za huko kumuhukumu mtu kwa makosa ya ukiukaji wa haki za binadamu,makosa yakiwa yamefanyika nje ya Marekani.

Mahakama moja mjini Miami imempata na hatia Charles Taylor Junior ambae kwa jina la kupanga anaitwa Chuckie.Hatia ni ya mashataka yote manane dhidi yake yaliyofanyika kati ya mwaka wa 1999 na mwaka wa 2003 nchini Liberia barani Afrika.Miongoni mwa madai hayo ni kuwa yeye na washirika wake waliwatesa watu nchini humo kwa kutumia vifaa kama kuwapigisha umeme katika sehemu zao za siri, kuwachoma kwa kutumia misumari ya moto pamoja na vipande vya plastiki.Isitoshe anatuhumiwa kwa shtaka la kupaka chumvi katika majeraha ya wahanga wake.

Inasemekana Taylor Junior mwenye umri wa miaka 31 alikuwa kamanda wa kikosi kilichokuwa kinapambana dhidi ya ugaidi kilichopewa jina la kupanga la 'vikosi vya shetani'.

Kikosi hicho kilikuwa kinamlinda babake Charles Taylor alipokuwa rais wa Liberia.Katika kisa kimoja inasemekana kuwa Taylor Junior alisimamisha kundi moja la watu ambalo lilishukiwa kuwa la waasi karibu na kituo cha barabarani kilichokuwa katika daraja la mto unaoitwa St Paul River.Inasemekana aliwachagua watu watatu kati yao na kuwauwa kwa kuwapiga risasi mbele ya wenzao.

Wahanga watano wa mateso hayo walitoa ushahidi wakati wa kusikizwa kesi hiyo dhidi ya Taylor junior, iliochukua mda wa wiki tano. Babake Taylor junior,Charles Taylor, anakabiliwa na mashataka ya uhalifu wa kivita uliodaiwa kufanyika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi jirani na Liberia ya Sierra Leone.Kesi hiyo inaendeshwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya mjini The Hague Uholanzi.

Mwendesha mashtaka wa Florida,Alexander Acosta,amesema kuwa baadhi ya mashahidi baado wana alama za mateso hayo, na kuongeza kuwa ingawa kesi hii ndio ya kwanza ya aina yake nchini humo lakini kuogeza kuwa hilo halimaanishi kuwa ndio kesi ya mwisho ya aina hiyo.

Tena naibu mwendesha mashtaka katika idara ya sheria ya Marekani, Sigal Mandelker, amesema kuwa hukumu hiyo ni ujumbe kwa wanaovunja haki za binadamu duniani kuwa hawatakiwi nchini humo.

Taylor Junior alizaliwa Boston Marekani.Jina lake la mwanzo lilikuwa Charles Emmanuel.Baadae mwaka wa 1990 alibadili ,kihahali, jina hilo na kuanza kuitwa Roy Belfast Junior ingawa alikuwa akijulikana kwa jina la kupanga kama Chuckie Taylor.Alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Boston mwaka wa 2006 na kukiri makosa ya kudanganya majina kamili ya babake katika makaratasi ya kuomba hati ya kusaifiria.Kabla ya kuhukumiwa alifunguliwa mashataka mapya ya kuwatesa watu.

Chuckie Taylor ni mtu wa kwanza kuhukumiwa katika sheria iliopitishwa mwaka wa 1994 nchini Marekani.Sheria hiyo inatoa ruhusa kumfungulia mshataka raia wa Marekani au mgeni akiwa nchini humo dhidi ya kuwatesa ama kuchangia kutesa watu nje ya Marekani.

Huku yake ni kifungo cha maisha.