1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtuhumiwa mwengine wa mashambulizi ya Brussels akamatwa

Mohammed Khelef25 Machi 2016

Polisi nchini Ubelgiji inasema imefanikiwa kumkamata mshukiwa mwengine wa mashambulizi ya kigaidi ya Jumanne mjini Brussels, huku kamata kamata ikiendelea kwa siku ya tatu mfululizo kote barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/1IJxG
Msako wa watuhumiwa wa ugaidi waendelea Brussels, Ubelgiji.
Msako wa watuhumiwa wa ugaidi waendelea Brussels, Ubelgiji.Picha: Reuters/V. Kessler

Mtu huyo amejeruhiwa kidogo na kutiwa nguvuni katika operesheni hiyo kaskazini mwa mji wa Brussels, na polisi inasema anahusika moja kwa moja na mashambulizi hayo ya Jumanne na pia jaribio lililoshindwa mjini Paris hapo jana.

Kituo cha habari cha Ubelgiji, RTL, kimeripoti kuwa polisi walimtaka mtu huyo avue koti lake akiwa kituo cha basi, huku mashahidi wakisema alikuwa amevaa mkanda wa mabomu.

Nchini Ufaransa, polisi inasema mshukiwa mwengine wanayemshikilia, kwa jina Reda Kriket, ana uhusiano wa moja kwa moja na mashambulizi ya Brussels. Kijana huyo wa miaka 34 alikutwa na silaha nzito na vifaa vya miripuko kwenye nyumba yake mjini Paris.

Hapa Ujerumani napo, polisi inamshikilia mwanamme wa Kimoroko mwenye umri wa miaka 28, ambaye ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu yake ya mkononi unahusishwa na mmoja wa washambuliaji wa kujitoa muhanga mjini Brussels.

Kijana huyo, ambaye alikuwa amezuiliwa kuingia kwenye mataifa yanayotumia mkataba wa Schengen, alikamatwa katika kitongoji cha Giessen, karibu na mji wa Frankfurt, na polisi waliokuwa wakipekua vitambulisho vya wasafiri kwenye kituo kimoja cha treni.

Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha ARD, simu ya kijana huyo ilionesha majina ya mmoja kati ya ndugu wawili, Ibrahim na Khalid el-Bakrawi, ambao wote walijiripua siku ya Jumanne, mmoja kwenye uwanja wa ndege na mwengine kituo cha treni cha Brussels, na kuuwa pamoja nao watu 31.

Polisi inasema dakika chache kabla ya miripuko mitatu kulikumba jiji la Brussels, mmoja wa washambuliaji hao aliwasiliana na mshukiwa huyo, kwa neno linalosomeka "fin" ikimaanisha "mwisho."

"Ugaidi wa kinyuklia"

Wakati huo huo, mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA), Yukiya Amano, akisema kuna haja kwa ulimwengu kufanya juhudi kubwa zaidi kuzuia kile alichokiita "ugaidi wa nyuklia", kwani kwa sasa haiwezi tena kupuuzwa kuwa magaidi hawataweza kuvifikia vifaa vya bomu hilo la maangamizi.

Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa, Yukiya Amano.
Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa, Yukiya Amano.Picha: Reuters/H.P. Bader

Akizungumza mjini Vienna kabla ya mkutano wa kilele juu ya nishati ya nyuklia unaofanyika Washington mwishoni mwa mwezi huu.

"Mataifa wanachama wanapaswa kuwa na maslahi ya pamoja na endelevu katika kuimarisha usalama wa nyuklia. Nchi ambazo hazitambui hatari ya ugaidi wa nykulia ndio tatizo kuu," alisema Amano.

Viongozi wa mataifa 50 duniani wanakutana kuanzia tarehe 31 Machi hadi 1 Aprili mjini Washington katika mkutano unaolenga kupendekeza mpango maalum wa kuvilinda vinu 1,000 vya atomiki duniani.

Uchunguzi wa polisi wa Ubelgiji mwezi Disemba mwaka jana, uligundua mkanda wa vidio wa masaa 10 juu ya nyendo za mmoja wa wataalamu wa nyuklia wa nchi hiyo kwenye nyumba ya mshukiwa wa mashambulizi ya Paris ya Novemba 2015, Mohamed Bakkali.

Magazeti nchini Ubelgiji yameripoti kwamba vidio hiyo ilichukuliwa na ndugu wawili, Khalid na Ibrahim, ambao walijiripua juzi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf