1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muafaka bado kupatikana juu ya nani ataiongoza serikali ya mpito ya Madagascar.

Halima Nyanza28 Agosti 2009

Mazungumzo ya kugawana madaraka kufuatia mzozo wa kisiasa ulioikumba Madagascar yamemalizika mjini Maputo, Msumbiji usiku wa kuamkia leo, licha ya kutofikiwa makubaliano yoyote ya jinsi ya kuunda serikali ya mpito.

https://p.dw.com/p/JJtF
Andry Rajoelina anasena nafasi ya Urais wa mpito Madagascar ni yake.Picha: AP

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Timu ya pamoja ya Kimataifa ya Usuluhishi wa mzozo huo, viongozi hao wa vyama vya kisiasa wanaowania nafasi ya uongozi katika serikali hiyo ya mpito ya Madagascar wameshindwa kufikia muafaka juu ya nafasi muhimu katika serikali hiyo ya mpito.

Hata hivyo, wasuluhishi katika mazungumzo hayo wamesema wanasiasa hao wamekubaliana kuondoa tofauti zao ifikapo Septemba nne kwa ajili ya kuwasilisha serikali mpya, katika kikao kijacho cha Jumuia ya nchi za Maendeleo kusini mwa Afrika SADC, kitakachoanza Septemba sita na kwamba tayari taasisi kadhaa katika serikali hiyo ya mpito zimeshaamuliwa.

Rais aliyeondolewa madarakani mwezi Machi mwaka huu, nchini Madagascar Marc Ravalomanana na kiongozi wa nchi hiyo kwa sasa Andry Rajoelina kila mmoja atachagua kiongozi wa moja ya mabaraza katika bunge la mpito.

Mahasimu hao wawili pia, kila mmoja atachagua Naibu Waziri Mkuu.

Taasisi nyingine katika serikali hiyo ya mpito zitaamuliwa na Rais wa zamani wa nchi hiyo Alberty Zafy na wajumbe wa vyama vya kiraia.

Bila ya makubaliano, hali haitakuwa nzuri Madagascar.

Akizungumza mara tu baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo bila ya muafaka, usiku wa kuamkia leo, Bwana Chisano amesema iwapo vyama vinavyoongozwa na viongozi hao wanne waliohudhuria mkutano huo vitashindwa kufikia muafaka, Jumuia ya Kimataifa itaitupa mkono nchi hiyo huku nchi wafadhili ,kutokuwa na haraka ya kubadili mtazamo wao kwa Madagascar.

Joaquim Chissano
Msuluhishi Mkuu wa mzozo wa kisiasa nchini Madagascar Joaquim Chissano.Picha: AP

Jumuia ya Kimataifa imeitenga Madagascar toka wakati huo, kuanza kwa mzozo huo, ikiwemo kukatiwa pia misaada, huku Umoja wa Afrika na Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC zikiisimamisha Madagascar uanachama wake hadi pale itakapofuata tena utawala wa sheria.

Viongozi hao wanaovutana nchini Madagascar pamoja na Marais wa zamani wa nchi hiyo Albert Zafy na Didier Ratsiraka walikubaliana katika mazungumzo ya awali yaliyofanyika Agosti 9 , kuteua majina ya viongozi watakaoshika nafasi katika serikali ya mpito, itakayoirudisha nchi hiyo katika utawala wa sheria kwa kufanya uchaguzi wa kidemokrasia mwishoni mwa mwaka ujao.

Wasuluhishi wakumbana na kibarua kigumu.

Wakati wa mazungumzo ya wiki hii wasuluhishi wa mzozo huo, walikumbana na kazi ngumu katika kuhakikisha usawa kati ya mahasimu hao katika kugawana nafasi za juu za uongozi za serikali hiyo ya mpito, ikiwemo nafasi ya Rais, Makamu wa Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mazungumzo hayo ya wiki hii yaliopangwa kufanyika kwa siku mbili yaliongezewa siku ya tatu ili kutoa nafasi kwa wanasiasa hao wanaopingana kutatua tofauti zao juu ya nafasi za juu za uongozi katika serikali hiyo ya mpito.

Chini ya Makubaliano yaliyofikiwa Agosti 9, Rais atakuwa ni mjumbe pekee katika serikali hiyo ya mpito kuweza kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwakani, huku Andry Rajoelina akisema ni yeye pekee atakayeweza kushika nafasi hiyo na kupingwa na Bwana Ravalomanana kwa kusema kuwa nafasi hiyo lazima iende kwa chama chake.

Nchi hiyo imekumbwa na mzozo wa kisiasa tokea aliyekuwa Meya wa mji wa Antananarivo Andry Rajoelina alipompindua madarakani Marc Ravolomanana akisaidia wa jeshi, baada ya wiki kadhaa za upinzani.

Katika makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wao wa Agosti 9 viongozi hao walitakiwa kutangaza majina ya serikali mpya katika kipindi cha siku 30.

Mwandishi: Halima Nyanza(AFP)

Mhariri: Abdul-Rahman